Wapalestina waandamana kulaani jinai za Wazayuni katika Masjidul Aqswa
Kundi la Wapalestina na wawakilishi wa makundi ya Palestina leo Jumapili wamefanya maandamano kulaani jinai za mara kwa mara zinazofanywa na Wazayuni maghasibu dhidi ya Msikiti wa Aqsa, Kibla cha Kwanza cha Waislamu.
Kituo cha upashaji habari cha Palestina kimeripoti kuwa, makumi ya Wapalestina wakazi wa Nablos katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na wawakilishi wa makundi mbalimbali ya Palestina wameshiriki kwenye maandamano hayo wakiwa wamebeba bendera za Palestina na kupiga nara za kulaani jinai za Wazayuni ikiwa ni kutangaza hasira zao kwa utawala wa Kizayuni. Waandamanaji hao wameunga mkono pia Wapalestina wanaoishi katika mji mtakatifu wa Baytul Muqaddas.
Siku ya Ijumaa Wapalestina waishio Ukanda wa Ghaza nao walifanya maandamano makubwa ya kulaani jinai ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuufunga Msikiti wa Aqsa.
Wakati huo huo leo Jumapili na baada ya kufunguliwa upya eneo la al Asbat la Masjidul Aqswa, mara kadhaa Wazayuni wamewafungia milango na kutowaruhusu kuingia msikitini humo Waislamu wa Palestina, jambo ambalo limewanyima Waislamu hao haki yao ya kutekeleza ibada ya Sala ya Aduhuri ndani ya Msikiti wa Aqsa.
Siku ya Ijumaa na baada ya vijana watatu wa Palestina kufanya opereseheni iliyo dhidi ya Wazayuni iliyopelekea Wapalestina watatu kuuawa shahidi na Wazayuni wawili kuangamizwa, Banjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni alitoa amri ya kufungwa Masjidul Aqswa.