Israel kujenga hospitali itakayotoa matibabu kwa magaidi wa Syria
Utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umekusudia kujenga hospitali katika miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na utawala huo nchini Syria, ambayo itakuwa na jukumu la kutoa matibabu kwa magaidi wanaopigana dhidi ya serikali ya Syria, ikiwa ni katika mwendelezo wa misaada ya utawala huo kwa magaidi hao.
Tomer Koller, afisa wa ngazi ya juu katika jeshi la Israel amefichua habari hiyo leo Alkhamisi na kuogeza kuwa, hospitali hiyo imepangwa kujengwa katika miinuko ya Golan ambayo inakaliwa kwa mabavu na utawala huo wa Kizayuni.
Koller amekiri kuwa, tangu mwaka 2011 kulipoanza machafuko nchini Syria hadi sasa, Israel imekwishawatibu magaidi 3000 wanaopigana kutaka kuiangusha serikali ya Syria baada ya kujeruhiwa na jeshi la nchi hiyo na kwamba mbali na matibabu hayo, Tel Aviv pia imekuwa ikiwasaidia magaidi hao kwa chakula, mavazi na mafuta. Kabla ya hapo Rais wa utawala haramu wa Israel, Reuven Rivlin sambamba na kukiri juu ya habari ya utawala wa Israel kuwapatia matibabu magaidi waliojeruhiwa nchini Syria ndani ya hospitali zake, alitaka kuongezwa misaada zaidi ya Tel Aviv kwa magaidi hao.
Utoaji matibabu wa Israel kwa makundi ya kigaidi wanaopigana kwa lengo la kuiangusha serikali ya Syria, ulishika kasi mwaka 2014 na hadi sasa bado unaendelea katika hospitali za utawala huo.