UN yatahadharisha kuhusu hali mbaya ya watoto milioni mbili wa Yemen
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuwa, watoto milioni mbili nchini Yemen wanakabiliwa na hali mbaya ya lishe duni, vita, umasikini na maradhi ya kipindupindu huku nchi hiyo ikakaribia kukabiliwa na ukame.
Asasi tatu za Umoja wa Mataifa za Shirika la Afya Duniani WHO, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF na Mpango wa Chakula Duniani WFP kwa pamoja zimetangaza katika taarifa yao hii leo kwamba, karibu asilimia 80 ya watoto wa Yemen wanahitajia misaada ya haraka ya kibinadamu huku maradhi ya kipindupindu nchini humo yakiwa yameshasababisha vifo vya karibu watu elfu mbili.
Taarifa ya mashirika hayo ya kimataifa imetahadharisha kwamba, watoto wanaokabiliwa na hali mbaya ya lishe duni wamekuwa rahisi kuugua kipindupindu. Kadhalika taarifa hiyo imetoa wito wa kutafutiwa ufumbuzi matatizo ya Yemen hususan suala la misaada ya kibinadamu ili kuiepusha nchi hiyo kukumbwa na maafa ya kibinadamu.
Hayo yanaripotiwa huku asasi mbalimbali za misaada ya kibinadamu zikitahadharisha kwamba, hali ya kibinadamu nchini Yemen inazidi kuwa mbaya siku baada ya siku huku kukiwa hakuna mataumaini ya kupatiwa ufumbuzi matatizo ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu.
Itakumbukwa kuwa, Saudia ilianzisha mashambulizi ya kila upande dhidi ya Yemen tangu mwezi Machi 2015 kupitia uungaji mkono wa madola ya Magharibi hususan Marekani, Uingereza, utawala haramu wa Kizayuni na baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo na kupitia siasa za kupenda kujitanua za watawala wa Aal Saud. Wayemen zaidi ya 13,000 wamepoteza maisha katika hujuma hiyo ya Saudia na waitifaki wake dhidi ya Yemen