Saudia imewanyonga watu 75 tangu ulipoanza mwaka huu
Wizara ya Mambo ya ndani ya Saudia imetangaza kuwa imewanyonga watu wengine wawili ambao ni raia mmoja wa nchi hiyo na mwengine wa Yemen na hivyo kuifanya idadi ya watu waliouliwa kwa njia hiyo ya kunyongwa nchini Saudia tangu mwanzoni mwa mwaka huu kufikia 75.
Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo, watu hao wawili wamenyongwa katika mji wa Asir, kusini mwa nchi hiyo. Shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International limekosoa vikali hukumu za kifo ambazo zimekuwa zikitekelezwa kila leo nchini Saudia na kusema kuwa si za kiadilifu na znakwenda kinyume na sheria za kimataifa. Kwa mujibu wa shirika hilo, Saudia imekuwa ikitekeleza hukumu hizo kwa lengo tu la kuwanyamanzisha wapinzani wa kisiasa na kwamba suala hilo linatia wasi wasi mkubwa. Ikumbukwe kuwa mwezi Januari pekee, utawala wa kifalme wa Aal-Saud uliwaua watu uliwaua watu 47 akiwemo Ayatullah Nimr Baqir an-Nimr, kiongozi wa Waislamu wa Kishia nchini Saudia. Hii ni katika hali ambayo Shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International lilikuwa limetangaza kuwa, utawala huo pia uliwanyonga vijana watatu walio na umri ulio chini ya miaka 18 kwa tuhuma tu za kushiriki katika maandamano dya kupinga utawala huo wa kidikteta unaoungwa mkono na madola ya Magharibi na hasa Marekani, suala ambalo linakinzana na sheria za kimataifa.