Magaidi wa Daesh kusafishwa kikamilifu Iraq, karibuni hivi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i33891-magaidi_wa_daesh_kusafishwa_kikamilifu_iraq_karibuni_hivi
Mbunge mmoja wa Iraq ambaye pia anashughulikia masuala ya usalama nchini humo amesema kuwa, karibuni hivi itaanza operesheni ya kuwafurusha magaidi wa Daesh katika ngome yao iliyobakia ya al Hawija na hivyo kuwasafisha kabisa magaidi hao nchini Iraq.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 02, 2017 21:59 UTC
  • Magaidi wa Daesh kusafishwa kikamilifu Iraq, karibuni hivi

Mbunge mmoja wa Iraq ambaye pia anashughulikia masuala ya usalama nchini humo amesema kuwa, karibuni hivi itaanza operesheni ya kuwafurusha magaidi wa Daesh katika ngome yao iliyobakia ya al Hawija na hivyo kuwasafisha kabisa magaidi hao nchini Iraq.

Mbunge huyo ambaye pia ni mjumbe wa kamisheni ya usalama na ulinzi ya bunge la Iraq amesema, ngome kuu iliyobakia ya magaidi wa ISIS ni mji wa Hawija katika mkoa wa Kirkuk kwenye jangwa la al Anbar la magharibi mwa Iraq na kwamba kuweko magaidi hao mjini humo kunahatarisha usalama wa maeneo mengine ya nchi hiyo kama vile Diyala na Baghdad.

Ameiambia televisheni ya al Sumaria ya Iraq kwamba, vikosi vyote vya ulinzi vya nchi hiyo vitashirikiana kwa karibu na wakazi wa mji huo katika operesheni ya kuwafurusha magaidi wa Daesh.

Helikopta ya kijeshi ya Iraq ikisambaza matangazo kwa ajili ya wakazi wa mji wa Hawija, mkoani Kirkuk

 

Amesisitiza kuwa, vikosi vya usalama na vya kijasusi vya Iraq vinakamilisha ukusanyaji wa taarifa ili kuwafungulia njia za kutoka mjini humo raia wasio na hatia kabla ya kuanza operesheni ya kuukomboa mji huo.

Siku ya Alkhamisi, kamati ya upashaji habari ya jeshi la Iraq ilisema kuwa, jeshi la nchi hiyo limesambaza matangazo kwa njia ya anga kuwatangazia wakazi wa mji wa Hawija kuwa karibuni hivi watakombolewa kutoka kwenye makucha ya magaidi wa ISIS. 

Kwa upande wake, Ahmad al Asadi, msemaji wa vikosi vya kujitolea vya wananchi maarufu kwa jina la al Hashd al Shaabi amesema kuwa, hivi sasa makumi ya maelfu ya wakazi wa mji wa Hawija wanadhibitiwa na magaidi wa Daesh na kwamba kuna wapiganaji wapatao elfu mbili wa ISIS katika mji huo.