Sisitizo la kulindwa umoja wa kitaifa nchini Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i33912-sisitizo_la_kulindwa_umoja_wa_kitaifa_nchini_iraq
Msimamo wa eneo la Kurdistan wa kutaka kuitisha kura ya maoni ya tarehe 25 mwezi huu kwa ajili ya kujitenga eneo hilo, umeendelea kukabiliwa na radiamali kali ya serikali ya Iraq, makundi tofauti ya nchi hiyo, nchi za eneo na ulimwengu mzima kwa ujumla.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Sep 03, 2017 23:49 UTC
  • Sisitizo la kulindwa umoja wa kitaifa nchini Iraq

Msimamo wa eneo la Kurdistan wa kutaka kuitisha kura ya maoni ya tarehe 25 mwezi huu kwa ajili ya kujitenga eneo hilo, umeendelea kukabiliwa na radiamali kali ya serikali ya Iraq, makundi tofauti ya nchi hiyo, nchi za eneo na ulimwengu mzima kwa ujumla.

Sayyid Ammar al-Hakim, Mkuu wa Chama 'Hikmat' nchini Iraq sambamba na kusisitiza juu ya umuhimu wa kulindwa umoja wa kitaifa wa taifa hilo amesema kuwa, kufanyika kwa kura hiyo ya maoni ya kulitenga eneo la Kurdiastan, hakuwezi kuhitimisha matatizo ya nchi hiyo. Sayyid Ammar al-Hakim ameongeza kuwa, kulindwa mahusiano ya kihistoria, ndiko kutaainisha mustakbali na fakhari ya Wakurdi, kuanzia viongozi wa kisiasa na raia wa kawaida. Kiongozi huyo wa chama cha 'Hikmat' amewatuhumu wale wanaoshabikia kutaka kuitishwa kura hiyo ya maoni kwa kusema: "Hii leo majirani wetu wote wamefahamu kuwa eneo lote limepatwa na taathira ya uthabiti na usalama wa Iraq." Mwisho wa kunukuu.

Sayyid Ammar al-Hakim, Mkuu wa Chama 'Hikmat' nchini Iraq

Huku viongozi wa eneo la Kurdistan nchini humo tayari wakiwa wameainisha tarehe 25 ya mwezi huu wa Septemba kuwa ndiyo siku ya kufanyika kura ya maoni ya kuamua imma kujitenga au kubakia eneo hilo ndani ya Iraq, kumeibuka tofauti za kisiasa ndani ya Kurdistan kwenyewe, tofauti ambazo zinatilia shaka sababu ya kufanyika kwa kura hiyo. Katika uwanja huo, msemaji wa harakati ya Mabadiliko ya 'Guran' ameweka wazi msimamo wake kwamba kufanyika kwa kura hiyo ya maoni ya kulitenga eneo la Kurdistan na Iraq, kutakuwa na madhara kwa raia wa ene hilo. Kabla ya hapo pia Haider al-Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq alikariri kwa mara nyingine msimamo wa serikali yake katika kupinga kuitishwa kura hiyo ya maoni na kusema kuwa: "Kuitishwa kura hiyo ya maoni uko kinyume cha sheria na umekosa vigezo." Tangu awali serikali ya Baghdad ilikuwa ikipinga kura hiyo ya maoni na kwamba suala hilo linakinzana na katiba ya Iraq.

Maoud Barzani ambaye kwa mashinikizo ya Israel na US anataka kujitenga

Wataalamu wa masuala ya kisiasa nchini Iraq wanaamini kuwa, kufanyika kura ya maoni ya eneo la Kurdistan ni utekelezaji wa njama za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na Marekani za kuigawa nchi hiyo ya Kiarabu yenye utajiri wa mafuta. Kufanyika kura ya maoni katika eneo hilo kunakokwenda sambamba na tofauti za ndani kati ya Wakurdi na kadhalika upinzani wa nchi za eneo hili kuhusiana na suala hilo, kunatajwa kuwa kutakakopelekea kuibuka mgogoro mkubwa katika eneo la Mashariki ya Kati. Kuhusiana na suala hilo, mtandao wa habari wa al-Quds al-Arabi umeandika makala kwa kumnukuu Bashiru Mussa Nafi kwamba: "Hatua ya eneo la Kurdistan ya kuitisha kura ya maoni, ni hatua ya kichokozi ambayo inaweza kusababisha kutokea vita." Mwisho wa kunukuu. Ni kwa ajili hiyo hatua yoyote ya kutaka kujitenga ya Wakurdi wa Iraq na Syria, itapelekea kuibuka vita vya umwagikaji damu mkubwa kwa kipindi cha miongo mingi ya baadaye.

Haider al-Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq

Mbali ni hayo ni kwamba sisitizo la eneo hilo la kuitisha kura hiyo, sambamba na kukabiliwa na radiamali kali ya kieneo na kimataifa na pia upinzani wa baadhi ya Wakurdi kuhusiana na suala hilo, linatazamiwa kuwa linaloweza kuibua vita vya ndani kati ya Wakurdi wenyewe suala ambalo halitatofautiana na hatma iliyoikumba Sudan Kusini. Ni kwa ajili hiyo ndio maana suala la kutaka kujitenga eneo la Kurdistan linatakiwa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo kati ya serikali kuu ya Baghdad, suala ambalo lingemalizika kwa gharama ndogo na kuzihakikishia nchi jirani na Iraq usalama wao. Kuhusiana na suala hilo, mtandao wa Intaneti wa Chuo Kidogo cha Carnegie umeandika makala kwa kumnukuu, Denis Natali akisema: "Masoud Barzani ameilipa Iraq gharama ya hatua yake ya kuitisha kura ya maoni kwa ajili ya kujitenga eneo la Kurdistan.

Bendera ya eneo la Kurdistan nchini Iraq

Hii ni kwa kuwa Barzani katika kujaribu kutatua matatizo ya ndani ya eneo hilo na kupunguza uwezo wa washindani wake wa kisiasa ndio akaamua kuitisha kura hiyo ya maoni, lakini pamoja kwa vyovyote iwavyo kura hiyo imefeli. Hivyo hatua yake ya kuendelea kushikilia msimamo wake huo haitakuwa na faida yoyote ghairi ya  kulivutia matatizo makubwa eneo hilo." Mwisho wa kunukuu. Ni suala lisilo na shaka kwamba, njama za kutaka kudhibiti eneo la Kirkuk na nusu ya mikoa ya Diyala, Salahud-Din na Nainawa zitalifanya eneo la Kurdistan kutumbukia katika vita vya umwagikaji mkubwa wa damu ambavyo si tu kwamba vitafelisha eneo hilo kuweza kujitenga, bali vitaandaa kutokea vita vya muda mrefu katika eneo hilo. Kuundwa serikali ya kikaumu nchini Iraq sawasawa iwe ni kwa matakwa ya raia, au kwa mapendekezo ya nchi za kigeni, kutasababisha kuibuka moto wa fitina katika eneo lote.