Jeshi la Syria lavunja mzingiro wa ISIS Deir ez-Zor
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i33950-jeshi_la_syria_lavunja_mzingiro_wa_isis_deir_ez_zor
Jeshi la Syria, likipata himaya ya wapiganaji waitifaki, limefanikiwa kufika katika mji wa Deir ez-Zor na kuvunja mzingiro wa miaka mitatu uliokuwa umewekwa na kundi la kigaidi la ISIS katika mji huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 05, 2017 09:32 UTC
  • Jeshi la Syria lavunja mzingiro wa ISIS Deir ez-Zor

Jeshi la Syria, likipata himaya ya wapiganaji waitifaki, limefanikiwa kufika katika mji wa Deir ez-Zor na kuvunja mzingiro wa miaka mitatu uliokuwa umewekwa na kundi la kigaidi la ISIS katika mji huo.

Televisheni ya kitaifa ya Syria imetangaza kuwa jeshi la nchi hiyo limeingia katika mji  huo leo Jumanne na sasa oparesheni ya kuondoa mabomu yaliyotegwa ardhini inaendelea. Duru zinasema kuna makabiliano makali yanayoendelea baina ya magaidi wa ISIS na jeshi la Syria.

Mapema leo Wizara ya Ulinzi ya Russia imetoa taarifa ikisema meli yake ya kivita iliyo katika Bahari ya Mediterranea imevurumisha makombora kadhaa ya Kalibr na kulenga mjumuiko wa magaidi wa ISIS karibu na mji wa Deir ez-Zor.

Wakati huo huo Rais Bashar al Assad wa Syria ametuma salamu zake za pongezi kwa jeshi la nchi hiyo kufuatua kufanikiwa kuvunja mzingiro wa ISIS mjini Deir ez-Zor.

Jeshi la Syria katika oparesheni dhidi ya ISIS

Magaidi wa ISIS waliteka eneo kubwa la mkoa wa Deir ez-Zor kati kati ya mwaka 2014 na kuchukua udhibiti wa visima vingi vya mafuta katika eneo hilo. Kukombolewa Deir ez-Zor kunamaanisha kuwa magaidi wa ISIS nchini Syria sasa watakuwa na ngome moja tu nchini humo ambayo ni mji wa Raqqa ambao nao pia unakarbia kukombolewa.