Dunia yaendelea kulaani jinai za Saudi Arabia nchini Yemen
Saudi Arabia na washirika wake wameendelea kufanya jinai na mauaji ya watu wasio na hatia nchini Yemen.
Ndege za kivita za Saudi Arabia mapema leo Jumamosi zimeshambulia maeneo ya kusini mwa mji mkuu wa Yemen, Sana'a na kuua raia kadhaa. Ndege hizo pia zimeshambulia kambi ya kijeshi ya Jabal al Nahdain na kandokando ya ikulu ya rais katika eneo la al Sab'in.
Mikoa ya Hajjah na Taezz pia haikusalimika na mashambulizi ya wavamizi wa Kisaudia na waitifaki wao. Wavamizi hao walianza kuishambulia Yemen mwezi Machi mwaka jana na hadi sasa Saudia na waitifaki wake wameua maelfu ya Waislamu wa Yemen na kuwalazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi. Vilevile asilimia 80 ya miundombinu ya nchi hiyo imeharibiwa kikamilifu kutokana na mashambulizi ya anga ya Saudia, na raia wa nchi hiyo wanasumbuliwa na uhaba wa huduma za afya, dawa, chakula na hata maji ya kunywa.
Ijumaa ya jana makumi ya maelfu ya wananchi wa Yemen waliandamana katika mji wa Sana'a wakipiga nara za kulaani utawala wa kifalme wa Saudia na Marekani. Waandamanaji hao wamelaani mashambulizi yaliyofanywa hivi karibuni na Saudi Arabia dhidi ya soko lililokuwa limefurika watu la al Khamis na kutoa wito wa kukomeshwa haraka mashambulizi hayo. Wananchi wa Yemen pia wameulaumu Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kwa ujumla kwa kutochukua hatua za maana dhidi ya jinai na ukatili wa Saudia Arabia. Katika mashambulizi hayo yaliyolenga soko katika mji wa Hajjah, watu wasiopungua 119 wameuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa.
Ni kutokana na mashambulizi kama hayo ndiyo maana Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zeid Ra'ad Zeid Al-Hussein, akasema kuwa maelfu ya raia wa kawaida wa Yemen wameuawa katika mashambulizi yanayofanywa na Saudia kwenye makazi ya raia. Zeid Al-Hussein pia amelaani vikali mauaji ya raia waliokuwa sokoni yaliyofanywa na ndege za Saudi Arabia huko kaskazini mwa Yemen na kusema kuwa, yameua watu wasiopungua 106 wakiwemo makumi ya watoto.
Kuhusu mauaji hayo ya watu waliokuwa sokoni, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa: Timu ya haki za binadamu haikupata ushahidi wowote wa kuwepo mapigano ya silaha au maeneo muhimu ya kijeshi katika eneo hilo wakati wa mashambulizi ya Saudi Arabia.
Wakati huo huo Ali Abdul Majiid ambaye ni mwanachama wa Idara ya Masuala ya Siasa ya harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema mahakama za nchi hiyo zina nyaraka zinazothibitisha kuwa, rais aliyejiuzulu na kutoroka nchi wa Yemen, Abd Rabbuh Mansur Hadi anaongoza vita na mashambulizi ya Saudia na ameunda makundi ya kigaidi nchini Yemen. Abdul Majiid ameongeza kuwa, watu wa Yemen wanafanya mikakati ya kumshtaki Abd Rabbuh Mansur Hadi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa sababu ya kuua watu wasio na hatia na kukandamiza mapinduzi ya amani ya Wayemeni.