UN yawataka wapinzani Syria kusalimu amri na kukubali kushindwa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i34035-un_yawataka_wapinzani_syria_kusalimu_amri_na_kukubali_kushindwa
Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Syria ameyataka makundi ya wapinzani katika nchi hiyo ya Kiarabu wasalimu amri na kutangaza kuwa yameshindwa katika mapambano yao ya kuiong'oa madarakani serikali ya Rais Bashar al-Assad.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 07, 2017 09:46 UTC
  • UN yawataka wapinzani Syria kusalimu amri na kukubali kushindwa

Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Syria ameyataka makundi ya wapinzani katika nchi hiyo ya Kiarabu wasalimu amri na kutangaza kuwa yameshindwa katika mapambano yao ya kuiong'oa madarakani serikali ya Rais Bashar al-Assad.

Staffan de Mistura amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kuwa, wapinzani wanafaa kufungua macho na kutizama mambo kwa uhalisia wake na kwamba vita nchini Syria vinaelekea ukingoni.

Amesema kwa sasa jambo la kuzingatiwa ni kuanzishwa mchakato wa kupatikana suluhisho la kudumu la kisiasa, na kusisitiza kwamba huo ndio utakuwa ushindi halisi.

Wanajeshi wa Syria wakisafisha ngome zilizobaki za Daesh

Kauli ya Mjumbe Maalumu wa UN inajiri baada ya jeshi la Syria Jumanne wiki hii kutangaza kuwa limefanikiwa kuvunja mzingiro katika mji wa Deir ez Zor mashariki mwa nchi hiyo ambao ulidhibitiwa na wanamgambo wa Daesh karibu miaka mitatu iliyopita.

Wadadisi wa mambo wanasema kuvunjwa mzingiro wa Deir ez Zor huko Syria ni mwanzo wa kukombolewa maeneo mengine yanayoshikiliwa na kundi la Daesh.

Mgogoro wa Syria ulianza mwaka 2011 kwa mashambulizi makubwa ya makundi ya kigaidi yanayosaidiwa na Saudi Arabia, Uturuki, Qatar, Marekani na Israel dhidi ya serikali halali ya nchi hiyo.