Saudia yalegeza kamba, haitaki eneo lolote la Syria lijitenge
Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia amesema kuwa, nchi yake na Russia zinaunga mkono umoja wa ardhi ya Syria na zinapinga jaribio lolote la kuigawa nchi hiyo.
Adel al Jubeir amedai kuwa, muda wote huu Riyadh imekuwa ikisisitizia udharura wa kulindwa umoja wa ardhi yote ya Syria.
Amesema, Saudia inataka uanze mchakato wa kisiasa nchini Syria kama ambavyo inaunga mkono pia juhudi za Russia za kutatua mgogoro wa Yemen.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia amezungumzia pia mgogoro ulioanzishwa na nchi yake dhidi ya Qatar na kusema kuwa msimamo wa Riyadh dhidi ya Doha hautobadilika mpaka Qatar itakapokubaliana na masharti ya Saudia.
Kwa upande wake, Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amenukuliwa na televisheni ya al Mayadeen ya Lebanon akizungumza na waandishi wa habari akiwa pamoja na waziri huyo wa mambo ya nje wa Saudia leo Jumapili mjini Jeddah akisema kwamba, Russia inasisitizia udharura wa kuundwa kamati ya pamoja ya wapinzani ambayo itaweza kufanya mazungumzo ya amani na serikali ya Syria.
Vile vile amesema, Moscow inafanya juhudi kubwa za kutatua mgogoro wa Qatar na nchi nne za Kiarabu na kuzitaka pande hizo zifanye mazungumzo ya moja kwa moja.
Itakumbukwa kuwa tarehe 5 Juni 2017, Saudia ilikuwa ya kwanza kutangaza kukata uhusiano wake wote na Qatar na kufunga mipaka yake yote. Muda mchache baadaye nchi za Misri, Imarati na Bahrain nazo zilijiunga na Saudia kukata uhusiano wao wa kila upande na Qatar.