Waziri Mkuu wa Iraq ametaka kusimamishwa kura ya maoni kuhusu Kurdistan
Haidar al Abadi Waziri Mkuu wa Iraq ametaka rasmi kusimamishwa kura ijayo ya maoni kuhusu kujitenga eneo la Kurdistan kufuatia serikali kuu kupinga vikali kura hiyo.
Al Abadi ametoa wito huo baada ya Mahakama Kuu ya Iraq jana Jumatatu kuagiza kuakhirisha kura hiyo ya maoni iliyopangwa kufanyika tarehe 25 mwezi huu ili kuchunguza kwanza iwapo zoezi hilo litakuwa la kikatiba au la.
Msemaji wa Mahakama Kuu ya Iraq Ayas al Samouk amesema kuwa mahakama imechukua uamuzi huo baada ya kupokea malalamiko ili kusitisha kufanyika kura hiyo ya maoni hadi pale zoezi hilo litakapochunguzwa na kubainika iwapo litakuwa ni la kikatiba au la.
Ijumaa iliyopita wabunge wa eneo la Kurdistan huko Iraq walipasisha kuendeshwa kura hiyo ya kujitenga eneo hilo licha ya kupingwa vikali na serikali kuu ya baghdad, Umoja wa Mataifa na Marekani.
Akizungumza katika mahojiano maalumu, Haidar al Abadi Waziri Mkuu wa Iraq amewatolea wito wa dhati viongozi wa eneo la Kurdistan kusimamisha zoezi hilo akisema kuwa uamuzi wa kutaka kuendesha kura ya maoni ni hatari na kuichukulia hatua hiyo kuwa sawa na kucheza na moto. Mwezi Juni mwaka huu Haidar al Abadi aliutaja uamuzi wa Mkuu wa serikali ya eneo la Kurdistan Masoud Barzani wa kutaka kuitisha kura hiyo ya maoni kuwa haukuchukuliwa katika wakati muafaka.