Yemen: Tunaweza kuvisambaratisha vituo vya kijeshi vya Israel huko Eritrea
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i35033-yemen_tunaweza_kuvisambaratisha_vituo_vya_kijeshi_vya_israel_huko_eritrea
Msemaji wa Jeshi la Yemen ameutahadharisha utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya kuendeleza chokochoko zake dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu akisisitiza kuwa, vituo vya kijeshi vya Tel Aviv vilivyoko nchini Eritrea vipo ndani ya shabaha ya makombora ya balestiki ya Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 30, 2017 04:37 UTC
  • Yemen: Tunaweza kuvisambaratisha vituo vya kijeshi vya Israel huko Eritrea

Msemaji wa Jeshi la Yemen ameutahadharisha utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya kuendeleza chokochoko zake dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu akisisitiza kuwa, vituo vya kijeshi vya Tel Aviv vilivyoko nchini Eritrea vipo ndani ya shabaha ya makombora ya balestiki ya Yemen.

Kanali Aziz Rashid ameiambia kanali ya televisheni ya al-Masira inayorusha matangazo yake kwa lugha ya Kiarabu kuwa: "Israel inashirikiana na Saudi Arabia katika mashambulizi ya anga dhidi ya Yemen. Tunaionya kuwa, makombora yetu ya balestiki yaliyoundiwa hapa nchini yana uwezo wa kuzilenga na kuzisambaratisha kambi za kijeshi za Tel Aviv zilizoko nchini Eritrea."

Kanali Aziz Rashid

Kamanda huyo wa ngazi za juu wa Yemen kadhalika ameuonya utawala haramu wa Israel kuwa makombora ya nchi hiyo ya Peninsula ya Kiarabu katika mustakabali wa hivi karibuni, yataimarishwa na kuwa na uwezo wa kuharibu bandari zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu, huko Paletina.

Mwezi Mei mwaka huu, duru za habari zilidokeza kuwa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilishirikiana na jeshi la Saudia katika kuhujumu eneo la Ta'izz nchini Yemen.

Ramani inayoonyesha namna Eritrea na Yemen zilivyogawanishwa na Ziwa Nyekundu

Kwa mujibu wa tovuti ya Liberty Fighters ya Uingereza , msemaji wa Jeshi la Saudi Arabia Meja Jenerali Ahmed al-Asiri alisema kuwa: "Skuadroni moja ya jeshi la Israel imehujumu kituo kimoja cha kutoa mafunzo cha kundi la Ansarullah katika mkoa wa Ta'izz na hivyo kutekeleza oparesheni yake ya kwanza." Mashambulio ya anga ya usiku na mchana ya Saudi Arabia dhidi ya Yemen, yaliyoanzishwa mwezi Machi mwaka 2015 na kuendelea hadi sasa yameshaua watu zaidi ya 13,000 na kuwafanya wengine zaidi ya milioni tatu wabaki bila ya makaazi.