Mar 22, 2016 06:54 UTC
  • Kugubikwa na wingu zito la hitilafu mazungumzo ya Syria Geneva

Huku wiki moja ikiwa imepita katika muda uliowekwa wa siku 10 kwa ajili ya mazungumzo ya amani ya Syria yanayofanyika mjini Geneva, hadi sasa hakuna chochote kilichoibuka kutoka ndani ya mazungumzo hayo, bali kwa mara nyengine tena wingu la hitilafu limetanda kwenye anga ya mazungumzo baina ya pande mbili husika.

Duru mpya ya mazungumzo ya Syria ilianza tarehe 14 mwezi huu wa Machi, na imepangwa kuendelea hadi tarehe 24.

Lakini baada ya kupita siku tano, mazungumzo hayo yalisita kwa muda wa siku mbili huku pande mbili za serikali ya Syria na wapinzani zikitazamiwa kukutana tena baada ya usitishaji huo.

Suala muhimu zaidi ambalo liko wazi hadi sasa ni kuwepo hitilafu nyingi baina ya pande mbili katika mazungumzo hususan juu ya uamuzi wa serikali ya Syria wa kuitisha uchaguzi wa bunge tarehe 13 Aprili, yaani takribani siku 20 kutoka sasa.

Kwa mujibu wa Yahya Qadhmani, naibu wa mratibu wa ujumbe wa wapinzani wa Syria, serikali ya Damascus imetaka mazungumzo hayo yaakhirishwe kwa muda wa wiki mbili ili kuipa fursa ya kukamilisha maandalizi ya uchaguzi huo. Hata hivyo ujumbe wa wapinzani umetangaza kuwa ikiwa mazungumzo hayo ya amani yataakhirishwa kwa ajili ya kufanyika uchaguzi wa bunge, ujumbe huo hautorudi tena kwenye meza ya mazungumzo.

Nukta muhimu ya kuzingatiwa hapa ni kwamba kuakhirishwa mara kwa mara mazungumzo ya Geneva hata kabla ya duru mpya ya tarehe 14 Machi kulikuwa kukisababishwa na hitilafu nyingi zilizokuwepo ndani ya kambi ya upinzani ambayo ndiyo iliyokuwa ikitoa wito huo wa kuakhirishwa mazungumzo hayo; lakini sasa wapinzani hao wanaituhumu serikali kuwa inataka kuakhirisha na kuchelewesha mchakato wa mazungumzo.

Nukta nyengine ni kwamba wachambuzi wengi wanaamini kuwa ikiwa pande mbili katika mazungumzo zitafikiria zaidi namna ya kuandaa na kuitisha uchaguzi wa bunge, mazungumzo yao yataweza kuwa na tija na faida zaidi na hata kuwezesha kuchukuliwa hatua za utangulizi za kuinasua Syria kwenye kinamasi cha mgogoro unaoikabili.

Inavyoonekana, mazungumzo ya sasa ya Geneva, kama yale ya Geneva 1 na 2 pamoja na vikao vya Moscow 1 na 2 hayatomalizika kwa kupatikana matokeo chanya kwa ajili ya kuutatua mgogoro wa Syria. Na sababu ya msingi ni kwamba japokuwa jumbe za mirengo ya upinzani zinapinga kuakhirishwa mazungumzo kwa muda wa wiki mbili lakini ukweli ni kuwa hakuna hata kimoja kati ya vikao kadhaa vilivyofanyika hadi sasa kuhusiana na mgogoro wa Syria, viwe ni vya kimataifa au baina ya Wasyria wenyewe kilichowezesha kukaribiana mitazamo ya serikali na ile ya wapinzani.

Mazungumzo yanayoendelea hivi sasa yanadhihirisha ufa mkubwa wa mpasuko uliopo baina ya pande mbili; na hitilafu juu ya suala la kuakhirisha kwa muda mfupi mazungumzo hayo ni cheche tu ya tatizo la msingi.

Upembuzi wa mgogoro wa Syria katika sura ya udhibiti wa mgogoro wenyewe unaonyesha kuwa kutokana na kushtadi hitilafu baina ya pande mbili, kuwepo uingiliaji mkubwa wa madola ya kigeni katika mgogoro huo yakiwemo ya eneo na ya kimataifa pamoja na kiini cha mgogoro wenyewe kuhusu namna ya muundo wa utawala na madaraka unavyopasa kuwa nchini humo, ni irada ya dhati ya kisiasa tu kupitia mazungumzo baina ya Wasyria wenyewe ndiyo itakayoweza kuhitimisha au angalau kupunguza ukubwa wa mgogoro wa miaka wa miaka mitano unaoendelea kuiteketeza Syria.../

Tags