Al-Abadi: Iraq itaendelea kuwa moja iliyoungana na yenye uthabiti
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i35808-al_abadi_iraq_itaendelea_kuwa_moja_iliyoungana_na_yenye_uthabiti
Waziri Mkuu wa Iraq Haidar Al Abadi ametangaza kuwa nchi hiyo itabaki kuwa moja na kwamba Iraq yenye uthabiti ni bora kwa uthabiti wa eneo la Mashariki ya Kati na dunia kwa jumla.
(last modified 2026-04-24T06:29:55+00:00 )
Oct 19, 2017 12:43 UTC
  • Al-Abadi: Iraq itaendelea kuwa moja iliyoungana na yenye uthabiti

Waziri Mkuu wa Iraq Haidar Al Abadi ametangaza kuwa nchi hiyo itabaki kuwa moja na kwamba Iraq yenye uthabiti ni bora kwa uthabiti wa eneo la Mashariki ya Kati na dunia kwa jumla.

Katika angalizo lake lililochapishwa kwenye toleo la leo la gazeti la New York Times la nchini Marekani, Al Abadi amesema Iraq inaweza kuthibitisha kuwa inao iwezo wa kutumia misingi ya demokrasia kwa ajili ya kutatua mizozo yake ya ndani.

Huku akibainisha kuwa katika wadhifa wake kama Waziri Mkuu inampasa ayalinde matabaka yote ya wananchi wa Iraq na kuhakikisha nchi inabaki imeungana, Haidar Al Abadi amesema: Ili kufikia lengo hili serikali imeimarishwa na imetekeleza kila kilichopasa kufanywa kwa mujibu wa sheria; kwa maana kwamba serikali ya shirikisho inabaki kuwa na mamlaka ya kusimamia mipaka ya kitaifa, usafirishaji mafuta na kudhibiti mapato ya forodha.

Vikosi vya Iraq baada ya kuudhibiti kikamilifu mji wa Kirkuk

Waziri Mkuu wa Iraq amesema kutumwa vikosi vya Iraq katika maeneo mbalimbali ya Kirkuk na maeneo mengine ya kaskazini mwa nchi kumefanyika kwa msingi huohuo na kuongeza kuwa: Vikosi vya serikali kuu vinaundwa na matabaka na jamii tofauti za kidini, kimadhehebu na kikabila nchini Iraq ikiwemo ya Wakurdi; na kusambazwa vikosi vya jeshi huko Kirkuk hakumaanishi hata chembe kuwa ni hatua ya kuwashambulia kijeshi raia wa Kikurdi au mji wenyewe wa Kirkuk.

Al Abadi amebainisha kuwa Kurdistan ya Iraq inakaribia kufilisika kwa sababu ya ufisadi wa kikundi cha viongozi wachache na familia zao. Waziri Mkuu wa Iraq aidha amewataka viongozi wa Kurdistan ya Iraq kuheshimu Katiba ya nchi na kuketi kwenye meza ya mazungumzo.../