Kamanda wa Badr: Itikadi za Kiwahabi zinachochea ugaidi
Kamanda wa kikosi cha wananchi wa Iraq cha Badr amesema kuwa Daesh na makundi mengine ya kigaidi katika eneo la Mashariki ya Kati yanaongozwa na fikra na itikadi za Kiwahabi za Saudi Arabia.
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano unaojadili mapambano dhidi ya Daesh unaoendelea katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad, Jenerali Hadi al-Ameri amesema kuwa, juhudi za kifikra zinahitajika kwa shabaha ya kukabiliana na itikadi na aidiolojia za makundi yenye misimamo ya kufurutu mipaka zinazochochea na kuhamasisha makundi ya kigaidi kama Daesh na al Qaida.
Amesema Daesh ni fikra potovu na kwamba uvamizi wa Marekani nchini Iraq mwaka wa 2003 ulichangia kukuza na kuimarisha itikadi na fikra za kundi hilo.
Saudi Arabia ambayo ndio makuu makuu ya fikra na itikadi za Kiwahabi inalaumiwa kwa kufadhili na kueneza aidiolojia hiyo potofu na isiyooana na mafundisho sahihi ya Uislamu.
Mwezi Machi mwaka huu afisa mmoja wa ngazi ya juu wa vyombo vya upelelezi nchini Iraq alisema kuwa asilimia 30 ya magaidi wa kundi la Daesh ni raia wa Saudi Arabia.
Aprili mwaka huu pia Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi alisema kuwa kila Muiraqi ana haki ya kuamini kwamba, Saudi Arabia inafadhili na kuyasaidia makundi ya kigaidi.