Qatar: Tutaimarisha na kulinda uhusiano wetu na Iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar amesema kuwa, Iran ni nchi jirani na nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi na kwamba Doha ina manufaa ya pamoja na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivyo haiwezi kukata uhusiano wake na Tehran.
Mohammed bin Abdulrahman Aal Thani amenukuliwa na shirika la habari la IRNA akisema hayo leo Jumatatu katika mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya TRT ya Uturuki na kusisitiza kwamba, uhusiano wa Qatar na Iran ni mzuri na hauwezi kuvurugwa na mashinikizo ya Saudi Arabia.
Amesema nchi zilizoiwekea vikwazo Qatar hadi hivi sasa zinaendeleza ugomvi na zinapinga kufanyika mazungumzo, bali zinatumia njia zisizo sahihi kufanikisha malengo yao.
Waziri huyo wa mambo ya nje wa Qatar pia amesema, upatanishi wa Kuwait katika mgogoro ulioanzishwa na Saudia na wenzake ni kitu cha kutegemewa na unaungwa mkono kimataifa na kwamba Doha iko tayari wakati wote kwa ajili ya mazungumzo ya kuutatua mgogoro huo.
Aidha amesema, hati ya Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi ina mapungufu mengi na ametaka hati hiyo iangaliwe upya. Amesema, hati hiyo imepoteza itibari yake na haikubaliki tena ila itakapofanyiwa mabadiliko ya kimsingi na kuwekwa wazi vipengee vyake vyote.
Itakumbukwa kuwa tarehe 5 Juni 2017, Saudi Arabia, Misri, Imarati na Bahrain ziliiwekea Qatar vikwazo vya kila upande vya angani, majini na ardhini na kuyafukuza mashirika na raia wa nchi hiyo katika nchi hizo kwa tuhuma kwamba Doha inaunga mkono ugaidi na haiko tayari kukata uhusiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.