Mkutano wa Kuwait, hatua nyingine ya kutengwa Israel na Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i36535-mkutano_wa_kuwait_hatua_nyingine_ya_kutengwa_israel_na_saudia
Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), Izzat al Rashq amesema kuwa, mkutano wa kukabiliana na hatua za koboresha uhusiano wa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi na utawala wa Kizayuni wa Israel uliofanyika Kuwait ni hatua muhimu katika njia ya kuitenga na kuiabisha zaidi Israel na washirika wake.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Nov 19, 2017 23:17 UTC
  • Mkutano wa Kuwait, hatua nyingine ya kutengwa Israel na Saudia

Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), Izzat al Rashq amesema kuwa, mkutano wa kukabiliana na hatua za koboresha uhusiano wa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi na utawala wa Kizayuni wa Israel uliofanyika Kuwait ni hatua muhimu katika njia ya kuitenga na kuiabisha zaidi Israel na washirika wake.

Mkutano huo umeitishwa na Harakati ya Kuisusia Israel ya Kuwait ikishirikiana na Harakati ya Vijana ya Kupinga Uhusiano na Israel ya Qatar na Taasisi ya Kukabiliana na Suala la Kuanzishwa Uhusiano na Israel ya Bahrain. Mkutano huo wa kukabiliana na suala la kuwepo uhusiano wa kawaida kati ya nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi na utawala haramu wa Israel ni jibu madhubuti dhidi ya harakati rasmi zinazofanywa na baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo hilo hususan Saudi Arabia za kupokea jumbe mbalimbali za Israel au kushirikiana nazo chini ya mwavuli wa kushirikishwa maafisa wa utawala huo haramu katika mikutano na shughuli mbalimbali za kimichezo, kiutamaduni na masuala ya kielimu.

Kwa msingi huo mkutano wa kupinga jitihada za kuanzishwa uhusiano na Israel katika nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi ni jibu na pigo kubwa kwa pande zinazofanya mikakati ya kuwepo uhusiano wa aina hiyo au zenye ndoto ya kuboresha uhusiano baina yao na utawala huo katili na kuuingiza kirahisi katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu. Nukta yenye umuhimu ni kuwa, mkutano huo umefanyika wakati ambapo maafisa wa Israel walikuwa wakidhani kwamba, katika kipindi cha sasa kumejitokeza mazingira mazuri zaidi ya kupenya na kuingia zaidi katika nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi. Hata hivyo kufanyika mkutano huo unaopinga suala la kuwepo uhusiano na Israel na kutoa wito wa kususiwa utawala huo katika nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi huko Kuwait kumevuruga kabisa mahesabu ya watawala wa Tel Aviv, Riyadh na mabwana zao.

Harakati ya kimataifa ya BDS inataka Israel isusiwe na kutengwa 

Harakati ya Kuitenga, Kuzuia Vitega Uchumi na Kuisusia Israel, BDS kwa kifupi ni harakati ya kimataifa ambayo lengo lake ni kuushinikiza utawala huo haramu kwa kutumia nyenzo za kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni ili ukomeshe kuikalia kwa mabavu ardhi ya Palestina na ubaguzi na kutambua rasmi haki ya mamilioni ya wakimbizi wa Palestina kurejea katika ardhi na nchi yao. Hivyo basi kufanyika mkutano wa Kuwait ambao kwa hakika ni nakala ya Kiarabu ya harakati ya BDS, ni ishara ya kuingia harakati hiyo katika mamlaka ya watawala wa Kiarabu wanaoota ndoto ya kuanzisha uhusiano rasmi na utawala katili na unaoua watoto wa Israel.

Image Caption

Mkutano huo unapata uhumu zaidi kwa kuzingatia kwamba, mwenyeji wake yaani Kuwait ni mwanachama wa Baraza la Ushirikiano wa nchi za Ghuba ya Uajemi linalodhibitiwa na Saudi Arabia. Suala hili lina maana kwamba, upinzani dhidi ya suala linalosisitizwa na Saudi Arabia la kuanzishwa uhusiano rasmi na Israel, sasa umeingia kwa nguvu katika nchi za Kiarabu wanachana wa baraza hilo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Waislamu wote wanalitambua suala la kuwa na uhusiano na utawala katili na unaoikalia kwa mabavu Quds tukufu na kibla chao cha kwanza kuwa ni mstari mwekundu ambao haupaswi kuvukwa na yeyeto.

Hali ya sasa ya kimataifa inaonesha kuwa, hakati ya kuzuia na kuitenga Israel, BDS kwa kifupi inayoungwa mkono na jumuiya za wafanyakazi, mashirika ya kiraia, taasisi zisizo za serikali na makundi ya kidini kote duniani, inaendelea kupanuka zaidi. Suala hili kwa upande wake ni kielelezo cha hasira na chuki za walimwengu dhidi ya siasa za kibaguzi za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Kwa kutilia maanani hali hii inaonekana kuwa, mikakati inayofanywa na Saudi Arabia ya kutaka kuwepo uhusiano wa kawaida kati ya nchi za Kiarabu na utawala haramu wa Israel haitakuwa na tija isipokuwa kuufedhehesha zaidi utawala huo wa kifalme na kuufanya utengwe zaidi.