Jan 17, 2026 02:30 UTC
  • Jumamosi, 17 Januari, 2026

Leo ni Jumamosi 27 Rajab 1447 Hijria sawa na 17 Januari 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1460 iliyopita, Mtume Mtukufu Muhammad Mustafa (s.a.w) alibaathiwa yaani kupewa Utume na Mwenyezi Mungu. Kipindi hicho Mtume Muhammad (s.a.w) alikuwa na umri wa miaka 40. Mtume Muhammad (saw) alianza kutafakari na kudurusu maumbile ya dunia akiwa bado mdogo na daima alikuwa akifirikia njia za kunyanyua juu utukufu wa mwanadamu. Alikuwa maarufu kwa ukweli, uaminifu na kutenda mema. Jumla ya sifa hizo njema zilimfanya Muhammad (s.a.w) kuwa shakhsia mwenye hadhi na heshima kubwa katika jamii. Alipitisha muda wake mwingi katika ibada na kutafakari katika Pango la Hiraa. Malaika Jibrail alimteremkia Muhammad akiwa katika pango hilo na kumpa bishara ya kwamba ameteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mtume wake kwa walimwengu wote. Tangu siku hiyo Mtukufu huyo alipewa jukumu kubwa la kuongoza wanadamu na kupambana na ujahili, ukafiri, dhulma na uonevu. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa siku hii adhimu.  ***

 

Siku kama ya leo miaka 980 iliyopita alizaliwa faqihi, mfasiri wa Qur'ani na msomi wa Kiislamu na Kiirani, Jarullah Zamakhshari. Mwanazuoni huyu pia alikuwa gwiji katika elimu za hadithi na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Msomi huyo wa Kiirani ameandika vitabu vingi vikiwemo vile vya Muqaddimatul Adab na Asasul Balagha. Kitabu muhimu zaidi cha Jarullah Zamakhshari ni tafsiri ya Qur'ani ya al "Kash'shaf". ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 219 iliyopita, aliaga dunia Sheikh Ja'afar Kashiful-Ghitaa msomi na fakihi mtajika wa Kiislamu. Alizaliwa mjini Najaf huko Iraq na kuanza kujihusisha na masomo ya dini tangu katika kipindi cha utoto wake. Awali alisoma masomo ya utangulizi kwa baba yake na kisha baadaye akahudhuria masomo kwa wasomi wakubwa wa zama hizo kama sayyid Mahdi Bahr al-Uluum. Baadaye Sheikh Ja'afar Kashiful-Ghitaa alianza kufundisha na kufanikiwa kulea wanafunzi wengi na vilevile kuandika vitabu vingi katika nyanja mbalimbali. *** 

 

Katika siku kama ya leo miaka 166 iliyopita, alizaliwa Anton Chekhov, mwandishi mashuhuri wa Urusi. Chekhov alizaliwa katika familia ya kipato cha chini na kupitia matatizo mbalimbali. Pamoja na hayo Anton Chekhov alifanya bidii kubwa ya masomo hususan katika fani ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Moscow na kuhitimu masomo yake chuoni hapo. Akiwa kijana alipendelea sana masuala ya uandishi na kuanza kujishughulisha na kazi za uandishi katika magazeti na wa makala tofauti za wakati huo. Alikuwa mahiri katika tenzi fupifupi na hivyo kutokea kuwa mashuhuri katika uga huo. Miongoni mwa athari za mwandishi huyo ni pamoja na kitabu cha "Jogoo wa Bahari" na vitabu vingine kadhaa. Anton Chekhov alifariki dunia nchini Ujerumani mwaka 1902.***

 

Tarehe 27 Dei miaka 70 iliyopita Navvab Safavi, mwanachuoni na mwanaharakati wa Iran aliuawa shahidi akiwa pamoja na wenzake watatu, baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifo kwenye mahakama ya kimaonyesho tu ya kijeshi katika utawala wa Shah hapa nchini. Akiwa kijana, Navvab Safavi alipata taaluma ya masomo ya kidini nchini Iran na kisha akaelekea Najaf nchini Iraq kwa shabaha ya kujipatia elimu zaidi. Alirejea nchini baada ya miaka kadhaa na kuanzisha mapambano dhidi ya utawala tegemezi na kibaraka wa Shah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo Safavi alikamatwa na utawala wa Shah na kuuawa shahidi akiwa na wenzake watatu.  *** 

 

Miaka 65 iliyopita katika siku kama hii ya leo aliuawa Patrice Lumumba mhandisi wa uhuru wa Kongo. Lumumba alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kukombolewa Kongo wakati wa harakati za ukombozi wa nchi za Kiafrika. Lumumba aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu na Waziri wa Ulinzi baada ya kuundwa Jamhuri ya Kongo mwaka 1960. Patrice Lumumba aliuawa mwaka 1961 na vibaraka wa Marekani na Ubelgiji baada ya kuvumilia mateso na unyama mkubwa. Mwanamapinduzi huyo shujaa aliandika vitabu kadhaa wakati wa uhai wake na mashuhuri zaidi ni kile alichokita "Kongo, Nchi Yangu."   ***  

 

Tarehe 17 Januari mwaka 1991 vikosi vya majeshi ya nchi kadhaa chini ya uongozi wa Marekani vilizishambulia ngome za wanajeshi wa Iraq huko Kuwait na Iraq ili kukomesha kukaliwa kwa mabavu Kuwait na jeshi la utawala wa Saddam. Mgogoro huo ulianza tarehe Pili mwezi Agosti mwaka 1990 baada ya utawala wa zamani wa Iraq kuikalila kwa mabavu ardhi ya Kuwait. *** 

 

Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita inayosadifiana na tarehe 27 Rajab 1415 Hijria, Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza kurusha hewani matangazo yake kwa mara ya kwanza. Matangazo ya Radio Tehran yalianza kurushwa kwa muda wa nusu saa tu nyakati za usiku, na yalifunguliwa kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kubaathiwa na kupewa Utume, Bwana wetu Muhammad (SAW).  Lengo la kuasisiwa Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kufikisha sauti ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa wananchi wanaodhulumiwa wa bara la Afrika, kuelimisha na kufichua njama za ubeberu wa kimataifa dhidi ya bara hilo. ***

 

Miaka 17 iliyopita katika siku kama ya leo, Wazayuni maghasibu walilazimika kutangaza usitishaji vita baada ya jeshi la utawala wa Israel kufanya mashambulizi ya kinyama ya siku 22 dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza. Katika mashambulizi hayo, utawala wa Kizayuni ulikusudia kuiangamiza Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas au kwa uchache kuilazimisha harakati hiyo ikubali mazungumzo eti ya mapatano. Hata hivyo uungaji mkono wa Wapalestina kwa harakati ya Hamas na vilevile malalamiko makali ya walimwengu dhidi ya jinai za wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza, yaliulazimisha utawala haramu wa Israel usitishe mashambulio yake.***