Kutangazwa ushindi wa mwisho wa taifa la Iraq dhidi ya ISIS
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i37447-kutangazwa_ushindi_wa_mwisho_wa_taifa_la_iraq_dhidi_ya_isis
Mkanda wa kuendelea kushindwa kundi la kigaidi la Daesh katika eneo la Mashariki ya Kati unaendelea kiasi kwamba, muda mchache baada ya kutangazwa kushindwa kikamilifu ISIS nchini Syria, habari nyingine zinasema kuwa magaidi hao wakufurishaji wameshindwa kikamilifu pia nchini Iraq.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Dec 11, 2017 00:04 UTC
  • Kutangazwa ushindi wa mwisho wa taifa la Iraq dhidi ya ISIS

Mkanda wa kuendelea kushindwa kundi la kigaidi la Daesh katika eneo la Mashariki ya Kati unaendelea kiasi kwamba, muda mchache baada ya kutangazwa kushindwa kikamilifu ISIS nchini Syria, habari nyingine zinasema kuwa magaidi hao wakufurishaji wameshindwa kikamilifu pia nchini Iraq.

Waziri Mkuu wa Iraq, Haydar al Abadi ametangaza rasmi habari hiyo na wakati huo huo kusisitiza kuwa, ushindi mkubwa zaidi ni kulindwa mshikamano na ardhi nzima ya Iraq na kuzuia kugawanyika vipande vipande nchi hiyo. Matamshi hayo yanaonesha ni kiasi gani viongozi wa Iraq wanalipa umuhimu mkubwa suala la kukabiliana na njama za maadui wa Iraq baada ya kusambaratishwa magaidi wa ISIS. Kutangazwa kushindwa kikamilifu Daesh nchini Iraq ni "jani jingine la dhahabu" katika historia ya taifa la Iraq ya kupambana na magaidi. Umoja, mshikamano na ushirikiano mkubwa uliooneshwa baina ya wananchi, jeshi na serikali ya Iraq ndiyo siri ya kufanikiwa taifa hilo katika kuliangamiza genge la Daesh. Hii ni katika hali ambayo, waungaji mkono wa magaidi hao yaani baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu wakiongozwa na Bani Saud wa Saudi Arabia na vile vile nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani bila ya kusahau utawala wa Kizayuni wa Israel, wote hao hawakuamini kabisa walipoona vibaraka wao wanasafishwa haraka mno katika nchi za Iraq na Syria. 

Haydar al Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq

 

Mwaka 2014, kundi la wakufurishaji la Daesh kwa uungaji mkono wa kifedha na kijeshi wa Marekani na waitifaki wake wa Magharibi na Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia, liliivamia Iraq na kuteka maeneo mengi ya kaskazini na magharibi mwa nchi hiyo ya Kiarabu na kuanza kufanya jinai za kutisha. Lakini mwamko wa wananchi wa Iraq kwa kushirikiana na jeshi na vikosi vya kujitolea vya wananchi vilifanikiwa kuwashinda nguvu na kuwafurusha magaidi hao katika ardhi yao na hivi sasa Waziri Mkuu wa Iraq, Haydar al Abadi ametangaza kwa fakhari kubwa kutokomezwa kikamilifu magaidi wa ISIS nchini humo. Hata hivyo, baada ya kuona njama yao iliyokuwa inatekelezwa na Daesh imeshindwa nchini Iraq, waungaji mkono wa magaidi hao hususan Marekani hawajakaa kimya bali wanaendeleza njama zao kwa mbinu tofauti ili kufifiliza ushindi mkubwa wa taifa la Iraq katika vita dhidi ya ugaidi. Mtandao wa Intaneti wa Marekani unaojulikana kwa jina la National Interest umechapisha maudhui iliyohusiana na kubadilika stratijia ya Daesh baada ya kushindwa nchini Iraq na Syria na kusema kuwa mikakati ya genge hilo hivi sasa ni kufanya harakati za chini kwa chini, za kutumia mitandao ya kijamii na pia kushadidisha mashambulizi ya kigaidi kama njia ya kuwatangazia walimwengu kuwa bado lipo.

Mbinu hiyo mpya magaidi katika eneo hili, nayo inaungwa mkono na Marekani na muungano unaodaiwa ni wa kupambana na ugaidi. Hivi sasa Wamarekani wameona kuwa njama zao zimeshindwa katika nchi za Iraq na Syria hivyo wanafanya njama za kila namna kuendeleza siasa zao za kibeberu katika nchi hizo na katika ulimwengu mzima wa Kiislamu. Kwa hakika rais wa Marekani Donald Trump ameshindwa kuzuia ushindi wa muqawama katika nchi za Syria na Iraq na kufeli huko kuna madhara makubwa kwa waungaji mkono wa magaidi katika eneo hili. Hivyo wanafanya njama za kila namna za kufifiliza ushindi huo wa kambi ya muqawama dhidi ya magaidi. Moja na njama zinazotumiwa ni hatua ya hivi karibuni ya rais wa Marekani ya kuitangaza Baytul Muqaddas kuwa eti ni mji mkuu wa dola pandikizi la Israel ili kuwashughulisha walimwengu na vitu vingine kabisa. Hata hivyo makosa yanayofanywa mara kwa mara na Trump katika siasa za kigeni yanashindana na makosa yake ya ndani ya Marekani ambayo yatakuwa na madhara makubwa kwa Marekani yenyewe kabla ya nchi nyingine yoyote.

Kusambaratika genge la wakufurishaji la ISIS (Daesh)

 

Hivi sasa upinzani na maandamano ya kuilaani ya Marekani yanaendelea katika kila kona ya dunia kutokana na Donald Trump kuitangaza Quds kuwa mji mkuu wa utawala wa Kizayuni. Hata Haydar al Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq wakati alipotangaza ushindi wa mwisho dhidi ya magaidi wa Daesh nchini humo amelaani uamuzi huo wa Trump na kusisita kuwa, hakuna mtu yeyote anayeweza kubadilisha utambulisho wa Quds ambayo ni ardhi isiyotenganishika na ardhi nyingine za Palestina. Hivi sasa Iraq iliyowatokomeza magaidi wa Daesh imejitokeza kwa uthubutu mkubwa kuilaumu Marekani kwa siasa zake za kuzusha machafuko na uungaji mkono wake kwa magaidi katika eneo hili ukiwemo utawala dhalimu wa Kizayuni na hilo ni pigo jingine kwa siasa za mambo ya nje za Marekani.