IOM: Zaidi ya nusu ya wakimbizi wa Kiiraqi wamerejea makwao
Shirika la Kimataifa kwa ajili ya Uhajiri (IOM) limetangaza kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Desemba wa mwaka uliomalizika wa 2017, wakimbizi milioni tatu, laki mbili na 20 elfu wa Kiiraqi walikuwa wamesharejea makwao.
Msemaji wa IOM Sandra Black ameashiria hatua zilizochukuliwa na vikosi vya jeshi la Iraq za kuyakomboa maeneo yaliyokuwa yamevamiwa na kukaliwa kwa mabavu na magaidi na kuboresha hali ya usalama katika maeneo hayo na kueleza kwamba: hadi mwishoni mwa mwaka 2015 ni wakimbizi laki tano tu wa Kiiraqi walikuwa wamerejea kwenye makazi yao, lakini hadi kufikia mwishoni mwa mwaka uliopita 2017 idadi hiyo ilifikia milioni moja na laki nane na nusu.
Kwa mujibu wa msemaji huyo wa Shirika la Kimataifa kwa ajili ya Uhajiri nchini Iraq, theluthi moja ya wahajiri wa Kiiraqi waliorudi kwenye eneo la makazi yao nyumba zao zote zilikuwa zimebomolewa kikamilifu.
Hapo kabla msemaji wa Wizara ya Uhajiri ya Iraq Sattar Nuruz alikuwa ametangaza kuwa asilimia 45 ya watu walioathiriwa na vita wamerejea kwenye makazi yao katika maeneo ya Mosul na Salahuddin huko kaskazini mwa Iraq pamoja na Diyala na An Anbar, mashariki na magharibi mwa nchi. Kwa mujibu wa Nuruz wakimbizi hao waliorejea makwao ni sehemu ya watu milioni tano ambao tangu mwezi Juni mwaka 2014 walilazimika kuzihama nyumba zao na kwenda kutafuta hifadhi kwenye makambi na maeneo ya usalama.../