Sisitizo la Lebanon kwa nchi za Kiarabu la kuishinikiza kidiplomasia Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i38551-sisitizo_la_lebanon_kwa_nchi_za_kiarabu_la_kuishinikiza_kidiplomasia_marekani
Kufuatia uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekkani dhidi ya Beitul-Muqaddas, Spika wa Bunge la Lebanon amesisitiza juu ya ulazima wa kufungwa balozi za nchi za Kiarabu nchini Marekani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 05, 2018 04:44 UTC
  • Sisitizo la Lebanon kwa nchi za Kiarabu la kuishinikiza kidiplomasia Marekani

Kufuatia uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekkani dhidi ya Beitul-Muqaddas, Spika wa Bunge la Lebanon amesisitiza juu ya ulazima wa kufungwa balozi za nchi za Kiarabu nchini Marekani.

Nabih Berri amesema kuwa, misimamo ya nchi za Kiarabu katika kukabiliana na hatua ya Marekani dhidi ya Quds ilikuwa dhaifu na kuongeza kwamba, uamuzi huo wa Washington unakiuka sheria, siasa na historia ya mji huo mtakatifu na vilevile maana yake ni kufunika uvamizi na jinai za Wazayuni huko Palestina.

Disemba 6 mwaka jana, Rais Donald Trump wa Marekani aliitangaza Beitul-Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala vamizi wa Israel, hatua ambayo ilifuatiwa na upinzani na radiamali kubwa ya walimwengu, viongozi na asasi za kimataifa. Kuhusiana na hilo, muamala wa kindumakuwili wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ulikosolewa vikali na walimwengu ikiwemo fikra za waliowengi katika nchi zenyewe za Kiarabu. Jumuiya hiyo ambayo ni marejeo rasmi ya kutetea na kuunga mkono maslahi ya Ulimwengu wa Kiarabu, ilichukua misimamo ya kidhalili mkabala na pigo kubwa kabisa lililotolewa na Marekani dhidi ya heshima ya ardhi nzima ya Palestina, Ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu.

Rais Donald Trump

Kikao cha dharura cha hivi karibuni cha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu huko Cairo Misri kilichoitishwa kwa shabaha ya kujadili uamuzi wa hivi karibuni wa Trump kuhusiana na kuutambua mji wa Beitul-Muqaddas kuwa mji mkuu wa Israel kilitoa taarifa dhaifu ambayo ilitosheka tu na kuitaka Marekani ifikirie upya uamuzi wake huo na ili kufikiwa hilo ikaitaka dunia iishinikize Washington.  

Wakati jumuiya hiyo ikionyesha msimamo huo dhaifu, nchi nyingine zimechukua misimamo dhabiti, imara zaidi na ya dhati dhidi ya hatua hiyo ya Trump. 

Gazeti la ar-Rai al-Yaum limeashiria katika toleo lake moja la mtandaoni msimamo dhaifu wa nchi za Kiarabu mkabala na uamuzi wa Rais Donald Trump kuhusiana na Beitul-Muqaddas na kuandika: Nchi hizo hazijamfukuza hata balozi mmoja wa Marekani au Israel kutoka katika miji mikuu yao na vile vile hazijamuita hata balozi mmoja wa Washington katika nchi zao ili kumkabidhi malamiko yao kwa hatua hiyo ya Trump.

Beitul-Muqaddas, Palestina

Ni jambo lililo wazi kwamba, kwa kuwa Donald Trump ni mfanyabiashara na ambaye anatanguliza mbele suala la chumo na faida, nchi za Kiarabu zingeweza kutumia hilo kumtikisa Trump lau kama zingesitisha makubaliano yao na Washington katika uga wa masuala ya kifedha, kibiashara na kidiplomasia.

Aidha kuwaita nyumbani mabalozi wa nchi za Kiarabu walioko Marekani na kuwatimua mabalozi wa Washington katika nchi za Kiarabu bado inaweza kuwa hatua athirifu na yenye kutoa indhari ya kidiplomasia kwa Donald Trump.

Katika fremu hiyo, fikra za waliowengi ulimwenguni zikiwemo za nchi za Kiarabu, zinataka kuchukuliwa maamuzi ya maana katika uwanja huo; na msimamo wa Nabih Berri, Spika wa Bunge la Lebanon unaakisi matakwa hayo.

Kikao cha Jumuiya ya Nchi za Kiarabu

Kwa kuzingatia unyeti ilionao kadhia ya Quds kwa Waplestina na kiujumla Ulimwengu wa Kiislamu, nchi za Kiarabu na fikra za waliowengi ulimwenguni, hatua yoyote ile ya kuwa pamoja na siasa za kupenda kujitanua za Israel huko Quds inaweza kuigharimu pakubwa Marekani kisiasa, kidiplomasia na kiuchumi.

Hapana shaka kuwa, hatua kama hiyo itakuwa sawa na kujilipua kisiasa na itaongeza msururu wa changamoto za Trump ambaye kutokana na siasa zake za ndani na za nje zilizozua makelele mengi anaandamwa na chuki za ndani na za kimataifa zinazoongezeka kila leo.

Kuongezeka miito ya kutaka zichukuliwe hatua za maana na nchi za Kiarabu dhidi ya Marekani kunaunga mkono na kutilia nguvu ukweli huu. Kiujumla ni kuwa, hatua ya Donald Trump ya kung'ang'ania kuwa na msimamo mmoja na Israel juu ya suala la kuendelezwa uvamizi wa Wazayuni dhidi ya Beitul-Muqaddas inaweza kukabiliwa na radiamali mbalimbali zikiwemo za kidiplomasia za nchi za Kiarabu na Kiislamu, ambapo natija ya hilo haitakuwa nyingine ghairi ya kutengwa zaidi Marekani kieneo na kimataifa.