Feb 22, 2018 04:29 UTC
  • Nabeel Rajab ahukumiwa kifungo cha miaka 5 jela nchini Bahrain

Nabeel Rajab, mwanaharakati mashuhuri wa masuala ya haki za binadamu nchini Bahrain amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kile kilichoelezwa kwamba, ni kupatikana na hatia ya uchochezi na jumbe za kukosoa utawala wa nchi hiyo.

Mahakama ya utawala wa Aal Khalifa nchini Bahrain ilitangaza jana kuwa, mwanaharakati huyo amehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kutokana na kuandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii  wa Facebook makala na matamshi ya ukosoaji.

Mahakama hiyo imeeleza kwamba, Nabeel Rajab amepatikana na hatia ya makosa mengi kama vile kutoa maneno ya kuivunjia heshima nchi jirani na kueneza uzushi katika kipindi cha vita.

Maandamano ya wananchi wa Bahrain dhidi ya utawala wa kifalme wa Aal Khalifa

Kwa mujibu wa mahakama hiyo, tuhuma hizo zinahusiana na maandishi yake yaliyoyaweka katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook mwaka 2015 ambapo alisema kuwa, utawala wa Bahrain umekuwa ukiwatesa wafungwa wa kisiasa. Aidha aliashiria mgogoro wa kibinadamu huko Yemen ambao alisema unasababishwa na mashambulizi ya kijeshi ya Saudi Arabia.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema kuwa, katika kipindi cha miaka sita  iliyopita, utawala wa kifalme wa Bahrain umekuwa ukiwatia mbaroni na kuwafunga jela wanaharakati mbalimbali wanaoikosia serikali ya nchi hiyo.

Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, katika kipindi cha miaka 6 iliyopita, zaidi ya raia elfu kumi na moja wa Baharain wamepokonywa uraia na kufukuzwa nchini humo kwa tuhuma zisizo na msingi wowote ule.

Tags