Onyo la Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq kwa Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amesema kuwa nchi hiyo itaendelea kupinga kuanzishwa vituo vya kijeshi vya Marekani katika ardhi ya nchi hiyo.
Siku ya Alkhamisi bunge la Iraq huku likizishukuru pande zote zilizolisaidia jeshi la nchi hiyo katika mapambano yake dhidi ya magaidi wa Daesh, limeitaka serikali ya Baghdad kuwasilisha jedwali la kuondoka askari wote wa kigeni walioko katika ardhi ya nchi hiyo. Vyanzo vya Iraq vinasema kwamba hivi sasa askari wapatao 9000 wa Marekani wapo katika ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu, ambapo inafanya juhudi kubwa za kuanzisha vituo vyake vya kudumu vya kijeshi nchini humo. Kwa mujibu wa shirika la habari la Irna, Ibrahim al-Ja'ffari, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, alisema Ijumaa usiku mwishoni mwa safari yake huko Moscow, Russia, kwamba Iraq haitafanya mzaha na nchi yoyote kuhusiana na udharura wa kuheshimiwa utawala wake.
Amesema hata baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia, kivuli cha vituo vya kijeshi vya Marekani kingali kinaonekana katika nchi za Korea Kusini, Uturuki, Japana na nchi nyingine nyingi za dunia, jambo ambalo amesema linakwenda kinyume na msingi wa kujitawala nchi hizo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq ameendelea kusema kuwa Iraq ilipoomba msaada wa askari wa kimataifa kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 2014 kwa ajili ya kupambana na genge la Daesh, iliwaambia wazi askari hao kwamba msaada huo haukupasa kukiuka mamlaka na kujitawala Iraq na kwamba ushirikiano wao katika jambo hilo haungeruhusiwa kupelekea kuanzishwa vituo vya kijeshi katika ardhi ya nchi hiyo. Huku akisisitiza kuwa kujitawala Iraq ni mstari mwekundu ambao hauwezi kujadiliwa, Ibrahim al-Ja'ffari amesema kuwa safari yake mjini Moscow imefanyika kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa Iraq na Russia.