EU yataka kukomeshwa mzingiro wa Ghaza
Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya ameutaka utawala wa Kizayuni wa Israel ukomeshe mara moja kuzikalia kwa mabavu ardhi za Palestina na pia uache kuuzingira Ukanda wa Ghaza.
Federica Mogherini jana Jumamosi alitoa tamko maalumu kuhusu jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina huko Ghaza na kuusisitizia wajibu wa kuheshimiwa haki na uhuru wa kujieleza wananchi hao kama ambavyo ameitaka Israel iache kuizingira Ghaza.
Tamko la Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya limesisitiza kuwa, uhuru wa kujieleza na haki za kijamii ni mambo ya msingi kabisa kwa kila mwanadamu hivyo ni wajibu kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kuheshimu haki hizo za Wapalestina.
Aidha Mogherini amesema, Umoja wa Ulaya unasisitizia msimamo wake wa kukomeshwa mzingiro wa Ghaza na kufungulia vivuko vyote vya kuingia na kutoka katika eneo hilo.
Jinai za utawala wa Kizayuni za kuwashambulia kinyama wananchi wa Palestina waliokuwa wanafanya maandamano ya amani ya kupigania haki zao zimeikasirisha sana jamii ya kimataifa kiasi kwamba hata marafiki wa Israel wamelazimika kulaani ukatili huo na kutaka kukomeshwa mara moja kuzingirwa Ukanda wa Ghaza.
Siku ya Ijumaa Wapalestina zaidi ya elfu kumi walifanya maandamano ya kupigania haki ya kurejea nchini kwao wakimbizi wa Kipalestina. Hata hivyo utawala wa Kizayuni wa Israel ulituma jeshi la askari zaidi ya elfu tatu ambao walitumia risasi za kivita, maguruneti na gesi za sumu kuwashambulia Wapalestina hao. Taarifa zinasema kuwa Wapalestina 17 waliuawa shahidi hiyo juzi na zaidi ya 1400 wengine walijeruhiwa.