Jeshi la Syria latangaza rasmi kukombolewa kikamilifu Ghouta Mashariki
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i42490-jeshi_la_syria_latangaza_rasmi_kukombolewa_kikamilifu_ghouta_mashariki
Jeshi la Syria limetangaza habari ya kukomboa kikamilifu eneo la Ghouta Mashariki, viungani mwa mji mkuu Damascus.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 01, 2018 02:59 UTC
  • Jeshi la Syria latangaza rasmi kukombolewa kikamilifu Ghouta Mashariki

Jeshi la Syria limetangaza habari ya kukomboa kikamilifu eneo la Ghouta Mashariki, viungani mwa mji mkuu Damascus.

Taarifa iliyotolewa na Kamandi Kuu ya Majeshi Yote ya Syria imesema kuwa, kufuatia mfululizo za operesheni za hali ya juu zilizofanywa na vikosi mbali mbali vya nchi hiyo, hatimaye eneo la Ghouta Mashariki limekombolewa kikamilifu toka mikononi mwa magenge ya kigaidi.

Jumatano iliyopita, wanajeshi wa Syria katika mji wa Harasta eneo la Ghouta Mashariki, walipata idadi kubwa ya mabomu yaliyotengenezwa na utawala haramu wa Israel katika mapango ya magaidi waliokuwa tayari wameshatoroka.

Kukombolewa eneo la Ghouta Mashariki kunatathminiwa kuwa na umuhimu mkubwa sawa na tukio la Jeshi la Syria kuukomboa mji wa Aleppo mwaka 2016.

Rais Bashar al-Assad aliwatembelea wakazi wa eneo la Ghouta Mashariki hivi karibuni

Eneo la kistratijia la Ghouta Mashariki lenye wakazi zaidi ya laki nne, limekuwa likitumiwa na magaidi kuvurumisha makombora katika mji mkuu wa Syria Damascus tokeo mwaka 2012, miezi michache baada ya Syria kutumbukia katika mgogoro.

Tokea mwaka 2011, Syria imekuwa ikikabiliana na makundi ya magaidi wakufurishaji na wanamgambo wanaopata himaya ya kigeni, hasa Marekani na Saudi Arabia. Katika miezi ya hivi karibuni, Jeshi la Syria, likipata msaada wa waitifaki wake, limefanikiwa kutoa pigo kubwa kwa magaidi nchini humo.