Saudia yaendeleza ukatili Yemen, yaua raia 15 katika shambulio jipya
Watu wasiopungua 15 wa familia moja wameuliwa katika shambulio lililofanywa na ndege za kivita za Saudi Arabia katika wilaya ya Dumnat Khadeer mkoani Taeez nchini Yemen.
Duru za habari zimeripoti kuwa, shambulio hilo la anga la jana Jumatatu pia limejeruhi raia wengine watano.
Hata hivyo baadhi ya duru za habari zimesema kuwa, waliouawa katika hujuma hiyo ya anga ya Saudia ni watu 17.
Shirika la habari la Mehr limesema yumkini idadi hiyo ikaongezeka kutokana na majeraha mabaya waliyoyapata wahanga wa shambulio hilo.
Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwezi Machi mwaka 2015 kwa uungaji mkono kamili wa Israel na baadhi ya nchi za Magharibi na za Kiarabu.
Hata hivyo mashambulizi hayo yameshindwa kufikia malengo yake ghairi ya kuua maelfu ya raia wasio na hatia.