Russia: Vikosi vya Syria vyaikomboa Douma na Ghouta yote ya Mashariki
Russia imesema kuwa jeshi la Syria limeukomboa mji wa Douma; mji wa mwisho huko Ghouta ya Mashariki kuwa chini ya udhibiti wa magaidi.
Mji huo umekombolewa katika kipindi cha chini ya miezi miwili tangu jeshi la Syria lianzishe oparesheni ya kuwafurusha magaidi katika mji huo karibu na mji mkuu wa Syria Damascus.
Meja Jenerali Yuri Yevtushenko Mkuu wa Kituo cha Amani na Suluhu cha Russia huko Syria amesema kuwa bendera ya Syria iliyopeperushwa katika jengo moja katika mji wa Douma ni ishara kwamba jeshi la Syria linadhibiti eneo hilo na Ghouta yote ya Mashariki. Eneo la Ghouta ya Mashariki limekuwa likitumiwa na magaidi kama kituo chao cha kuanzishia mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu mbalimbali huko Damascus. Inafaa kuashiria hapa kuwa jeshi la Russia limekuwa likiipatia Syria msaada wa ndege za kivita katika oparesheni yake dhidi ya magaidi iliyoanza Februari 19 mwaka huu.
Katika upande mwingine, jeshi la Syria jana liliripoti kuwatia mbaroni wanajeshi kadhaa wa Uingereza kufuatia oparesheni iliyoanza kutekelezwa na jeshi huko Ghouta ya Mashariki tangu tarehe 26 Februari mwaka huu kwa lengo la kuwaangamiza magaidi katike eneo hilo na kuwasaidia wananchi wa Syria.