Kukosolewa jinai zinazoendelea kufanywa na Saudia dhidi ya wananchi wa Yemen
Mfalme Salman bin Abdul aziz wa Saudi Arabia amepuuza na kudharau maonyo yanayotolewa kimataifa yakiwemo ya asasi za kutetea haki za binadamu na kuamua kuendeleza jinai zake dhidi ya wananchi wa Yemen.
Shirka la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa ripoti, ambapo mbali na kukosoa kuendelea mashamulio ya Saudia nchini Yemen limetangaza kuwa tangu Machi 25 mwaka jana, Riyadh imekuwa ikiendeleza wimbi la mashambulio dhidi ya maeneo mbalimbali ya Yemen kwa lengo la kumrejesha madarakani Rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu Abd Rabbuh Mansur Hadi. Ripoti ya Human Rights Watch imefafanua kuwa hadi sasa maelfu ya raia wamepoteza maisha, na hasara ya mabilioni ya dola imesababishwa kwa miundombinu ya Yemen kutokana na mashambulio hayo.
Katika ripoti hiyo iliyotolewa siku ya Ijumaa na Sarah Leah Whitson, Mkurugenzi wa shirika hilo la kutetea haki za binadamu katika Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini imeelezwa pia kwamba ukiukaji wa sheria za kimataifa uliofanywa na Saudia nchini Yemen hauwezi kukanushika, kwa sababu Riyadh imeshambulia maeneo ya makazi ya raia na kutumia mara kadhaa katika mashambulio hayo silaha zilizopigwa marufuku yakiwemo mabomu ya vishada na ya fosferi.
Ripoti ya Human Rights Watch imeendelea kueleza kuwa Marekani na Uingereza ni waungaji mkono wa Saudia na waitifaki wake katika mashambulio yao dhidi ya Yemen kutokana na kuuzia utawala wa Kifalme wa Aal Saud silaha na zana za kijeshi zenye gharama ya mabilioni ya dola.
Hapo kabla, Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International nalo pia lilitoa taarifa ya kulaani mauaji ya raia wa Yemen yanayofanywa na jeshi la Saudia na kuzitaka Marekani na Uingereza zisitishe kuuuzia silaha utawala wa Aal Saud, kwa sababu silaha hizo zinatumiwa kuulia raia wasio na hatia wa Yemen.
Licha ya asasi za kimataifa za kutetea haki za binadamu kukosoa na kufichua nafasi ya baadhi ya nchi zikiwemo Marekani na Uingereza katika mashambulio yanayofanywa na Saudia dhidi ya Yemen, utawala wa Aal Saud ambao umeunda muungano wake bandia ulioupa jina la 'Muungano wa Kiarabu' ungali unaendelea kufanya jinai nchini Yemen.
Jinai hizo zinaendelea kufanywa katika hali ambayo Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limetaka mara kadhaa kufanya uchunguzi huru kuhusu ukiukaji wa sheria za vita uliofanywa nchini Yemen, lakini jitihada zake zimegonga mwamba kutokana na ukwamishaji uliofanywa na baadhi ya nchi zikiwemo Marekani na Uingereza.
Wachambuzi wanasema, madamu Marekani, Uingereza na waitifaki wao ukiwemo utawala wa Kizayuni wa Israel zinafaidika na vita hivyo, wananchi madhulumu wa Yemen wataendelea kuwa wahanga wa sera za kujipanua za utawala wa Aal Saud na waungaji mkono wake.
Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa mashambulio ya kinyama yanayoendelea kufanywa na Saudia dhidi ya Yemen hadi sasa yameshaua zaidi ya watu 8,400 wakiwemo watoto 2,236 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 16,000. Mashambulio hayo yamesababisha hasara kubwa pia kwa miundombinu ya nchi hiyo ambapo majengo mengi ya hospitali, skuli na viwanda yamebolewa kikamilifu.../