Mapatano ya Karne; mpango wa kuifuta Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i43940-mapatano_ya_karne_mpango_wa_kuifuta_palestina
Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani yay Palestina amesisitiza kuwa, Beitul-Muqaddas ni mji mkuu wa abadi na milele wa Palestina.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 02, 2018 08:07 UTC
  • Mapatano ya Karne; mpango wa kuifuta Palestina

Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani yay Palestina amesisitiza kuwa, Beitul-Muqaddas ni mji mkuu wa abadi na milele wa Palestina.

Sisitizo hilo la Mahmoud Abbas ni muendelezo wa radiamali za Wapalestina kwa njama za Marekani dhidi ya mji wa Quds na vizingiti vya Washington katika njia ya kuasisiwa dola na nchi huru ya Palestina mji mkuu wake ukiwa ni Beitul-Muqaddas.

Rais Mahmoud Abbas sambamba na kulaani na kuyapinga maneno yanayohusiana na 'Mapatano ya Karne' amesisitiza kwamba, hakuna wakati ambao muamala na mapatano kama hayo yatakubaliwa. Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kadhalika amesisitiza kwamba, hataikubali nchi ya Palestina yenye mipaka ya muda.

Baada ya kuingia madarakani Rais Donald Trump wa Marekani wigo wa chuki na uhasama wa Washington dhidi ya Palestina umepanuka na kuwa wa hatari zaidi. Kuzungumziwa mpango wenye njama wa Donald Trump wenye anuani ya 'Mapatano ya Karne' ni jambo ambalo linazidi kudhihirisha ukubwa wa njama za kila upande za Washington dhidi ya Wapalestina. 

Rais Donald Trump wa Marekani akiwa na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel

Kwa mtazamo wa fikra za waliowengi pamoja na duru za kisiasa katika eneo la Mashariki ya Kati ni kuwa, Mapatano ya Karne ni mpango wenye shabaha ya kuifuta kikamilifu kadhia ya Palestina. Ni katika fremu ya mpango huo huo, ndipo Rais Donald Trump Disemba 6 mwaka jana akaitangaza Beitul-Muqaddas kuwa mji mkuu wa utawala haramu wa Israel.

Aidha Trump alitangaza uamuzi wake wa kuhamisha ubalozi wa nchi yake huko Tel Aviv na kuupeleka Beitul-Muqaddas, hatua ambayo ilikabiliwa na malalamiko na upinzani mkali wa Wapalestina na kulaaniwa kieneo na kimataifa. Kwa kuzingatia muundo wa mpango wa Trump ulivyo katika kuhitimisha mgogoro wa Palestina kwa maslahi na manufaa ya utawala wa Kizayuni wa Israel, mpango wake huo unahesabiwa kuwa hatari zaidi kuwahi kupendekezwa na Marekani hadi sasa kwa ajili ya kutokomeza malengo matukufu ya Palestina na hivyo kulifunga faili la Palestina kwa maslahi ya utawala ghasibu wa Israel.

Hatua hiyo ya Trump imelipua ghadhabu za fikra za waliowengi na kupelekea kuchukua wigo mpana zaidi malalamiko ya Wapalestina. Maandamano ya 'Haki ya Kurejea' ambayo yamekuwa yakishuhudiwa kwa wiki kadhaa sasa huko Palestina nayo ni radiamali ya Wapalestina kwa njama za Marekani. Mahir Tahir mmoja wa wanaharakti wa Kipalestina sanjari na kulaani mpango wa mapatano wa Marekani unaojulikana kama 'Mapatano ya Karne' kuhusiana na Palestina amesema kuwa, mpango huo umezaliwa ukiwa mfu, hivyo hauwezi kupiga hatua na kusonga mbele.

Mji wa Quds

Mahir amesisitiza kwamba, umewadia wakati sasa kwa makundi ya Kipalestina kushikamana na kuwa kitu kimoja na hivyo kukabiliana na Trump, Waarabu wenye fikra mgando pamoja na mpango huo wa 'Mapatano ya Karne.

Kwa mujibu wa mpango huo, masuala kama kuweko uhusiano wa kawaida baina ya nchi za Kiarabu na Israel, kufutwa haki ya kurejea katika ardhi za Palestina wakimbizi wa Kipalestina, kufumbiwa macho kadhia ya mateka wa Kipalestina na kukanyagwa haki za Wapalestina katika mji wa Quds ni mambo yanayofuatiliwa ndani ya mpango huo. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana mpango huo umekabiliwa na malalamiko mengi ya fikra za waliwengi ulimwenguni.

Hata hivyo viongozi wa Marekani wamepuuza malalamiko hayo huku wakiendeleza njama zao dhidi ya Wapalestina. Kwa msingi huo, viongozi wa Marekani wanaamini kuwa, kama kwa upande wa kisiasa kuundwa nchi ya Palestina litakuwa jambo la dharura na lisiloepukika basi fikra hiyo inapaswa kuwa ya muda na sio ya daima ili katika kipindi cha muda mrefu iwezekane kuitokomeza fikra ya kuundwa nchi huru ya Palestina.

Ramani inavyoonyesha jinsi Israel ilivyopora hatua kwa hatua ardhi ya Palestina

Katika uwanja huo, Marekani kwa kutoa masharti kama vile, nchi ya Palestina inapaswa kuwa  na mipaka maalumu na ya muda, isiyo na jeshi na vile vile kwa upande wa siasa za kigeni, mipaka na mamlaka yake ya anga ni mambo ambayo yanapaswa kuwa chini ya usimamizi wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel, inakusudia kufuatilia malengo yake haramu dhidi ya kadhia ya Palestina. 

Hapana shaka kuwa, masharti hayo ya Marekani hayawezi kukidhi masharti ya kuasisiwa nchi yenye mamlaka. Kwa msingi huo basi, njama tofauti za viongozi wa Marekani zinalenga kuzuia kufikiwa malengo matukufu ya Palestina.