Saudia yaendelea kurundika silaha, yatumia dola bilioni 69 mwaka jana pekee
Ripoti mpya ya Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI) inaonyesha kuwa, fedha zinazotengwa na baadhi ya nchi ikiwemo Saudi Arabia kwa sababu za kijeshi mwaka jana 2017 zimeongzeka kwa asilimia 1.1, sawa na dola trilioni 1.739 za Marekani.
Ripoti hiyo iliyotolewa jana Jumatano imeonyesha kuwa, Saudia ni kati ya nchi tatu zilizoongoza kwa ununuzi wa silaha mwaka jana, katika hali ambayo Riyadh imeendelea kushadidisha mashambulizi yake na waitifaki wake dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya SIPRI, Saudi Arabia imeshika nafasi ya tatu iliyokuwa ikishikiliwa na Russia mwaka juzi, katika kuelekeza mapato yake mengi kwenye matumizi ya kijeshi na hususan ununuzi wa silaha.
Ripoti hiyo mpya ya Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm imebainisha kuwa, utawala wa Aal-Saud mwaka jana ulitumia zaidi ya dola bilioni 69.4 kujiimarisha kijeshi, nyuma ya China iliyotumia dola bilioni 228 na kushika nafasi ya pili.
Marekani imeendelea kuwa nchi inayoongoza kwa kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya masuala ya kijeshi, ambapo mwaka jana 2017 ilitumia dola bilioni 610.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, dunia ilitumia dola trilioni 1.73 mwaka jana pekee katika masuala ya kijeshi.
Mwezi uliopita wa Aprili pekee, Washington ilikubali kuiuzia Riyadh mifumo 180 ya mizinga yenye thamani ya dola bilioni 1.31 ikiwa ni katika muendelezo wa Marekani wa kuiuzia Saudia silaha za mabilioni ya dola.
Itakumbukwa kwamba, akiwa ziarani mjini Riyadh mwaka jana wa 2017, Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa, Saudi Arabia itanunua silaha zenye thamani ya dola bilioni 110 kutoka Marekani.