HRW: Benki za Israel zinafadhili jinai za kivita dhidi ya Wapalestina
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limesema benki za Israel zinafadhili jinai za kivita za utawala huo wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.
Ripoti ya kurasa 41 iliyochapishwa jana na shirika hilo lenye makao makuu yake mjini New York Marekani imesema benki hizo zinafadhili ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, jambo ambalo linachangia uvunjaji wa haki za binadamu na jinai za kivita dhidi ya Wapalestina.
Sari Bashi, Mkurugenzi wa Palestina na Israel wa shirika hilo amesema kuwa, "Benki za Israel zinashirikiana na wawekezaji kuwatengenezea nyumba Waisraeli katika ardhi za Palestina."
Ameongeza kuwa, kitendo hicho cha Israel cha kupanua ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Wapalestina ni sawa na jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu.
Hatua hiyo inafanyika katika hali ambayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tarehe 23 Disemba 2016 lilipitisha azimio ambalo linautaka utawala wa Israel kuhitimisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi katika ardhi za Palestina.
Akitoa radiamali yake juu ya ripoti ya Human Rights Watch, Saeb Erekat, Katibu Mkuu wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) amesema Mamlaka ya Ndani ya Palestina itachukua hatua zinazostahili dhidi ya benki hizo za Israel, kwa kukiuka haki za Wapalestina.