Jun 20, 2018 16:19 UTC
  • Polisi wa Iraq wagundua mahandaki mawili ya magaidi wa Daesh (ISIS)

Polisi wa Federali ya Iraq imetangaza leo kuwa, imefanikiwa kugundua mahandaki mawili ya genge la kigaidi la Daesh (ISIS) katika eneo la Khuwaja na kutegua zaidi ya mabomu 10 yaliyokuwa yametegwa kwenye mahandaki hayo.

Shirika la habari la Iraq limemnukuu Meja Jenerali Shakir Jodat, kamanda wa polisi ya shirikisho la Iraq akitangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, brigedi ya wahandisi wa Polisi ya Federali wamefanikiwa kutegua mabomu 9 na kugundua vifurushi vitatu vilivyotegwa mabomu.

Amesema baada ya jeshi hilo kupata taarifa za kijasusi za kuingia kundi moja la magaidi katika eneo la Ali Daham huko Kirkuk, lilianzisha mara moja operesheni ya kuwasaka magaidi hao na kuwatia mbaroni magaidi wawili katika eneo la Tard Nasir. 

Daesh (ISIS)

 

Jeshi la Polisi ya Federali ya Iraq aidha limesema limefanikiwa kukamata kifaa cha kutesea watu kwa kutumia umeme kilichokuwa kinatumiwa na magaidi kuwatesa mateka wao.

Tarehe 21 Disemba 2017, serikali ya Iraq ilitangaza rasmi kusafishwa kabisa magaidi wa ISIS nchini humo lakini wakati huo huo ilitangaza kuwa, mabaki ya magaidi hao wamejificha katika maeneo tofauti wakisubiri fursa ya kufanya uhalifu hivyo kuwataka wananchi wote wa Iraq kushirikiana na maafisa usalama wa nchi hiyo na kutoa taarifa kwa vyombo husika kila wanapoona kitu kisicho cha kawaida au wanapowashuku watu.

Tags