Utawala wa Kizayuni kubomoa nyumba 50 za Wapalestina Ukingo wa Magharibi
Utawala wa Kizayuni wa Israel umetishia kubomoa zaidi ya nyumba 50 za Wapalestina kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, ikiwa ni muendelezo wa sera kandamizi za Tel Aviv katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu kinyume cha sheria za kimataifa.
Vyombo vya habari nchini Palestina vimeripoti kuwa, utawala huo haramu unapanga kubomoa makumi ya nyumba hizo za Wapalestina katika kijiji cha Beit Dajan, kilichoko mashariki mwa mji wa Nablus.
Nasir Abu Jaish, Meya wa eneo hilo amesema jeshi la utawala ghasibu wa Israel tayari limewapa ilani ya siku 60 wakazi wa nyumba 51 katika kijiji hicho, eti kwa kujenga bila vibali.
Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni utawala khabithi wa Israel uliafiki pendekezo la ujenzi za nyumba zaidi ya 1000 katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, mbali na mpango wa ujenzi wa nyumba zingine 2500 katika maeneo tofauti ya Palestina.
Hatua hiyo inafanyika katika hali ambayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tarehe 23 Disemba 2016 lilipitisha azimio ambalo linautaka utawala wa Israel kuhitimisha ujenzi wa vitongoji vya walowezi katika ardhi za Palestina.