Waandamanaji wa Kipalestina watungua drone ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i46489-waandamanaji_wa_kipalestina_watungua_drone_ya_israel
Waandamanaji wa Kipalestina wamedondosha ndege ya kijasusi isiyo na rubani ya utawala wa Kizayuni wa Israel, katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 01, 2018 02:49 UTC
  • Waandamanaji wa Kipalestina watungua drone ya Israel

Waandamanaji wa Kipalestina wamedondosha ndege ya kijasusi isiyo na rubani ya utawala wa Kizayuni wa Israel, katika Ukanda wa Gaza.

Duru za habari zimeripoti kwamba drone hiyo ya kijasusi ya Israel ilitunguliwa jana Jumamosi, wakati ikichunguza nyendo na harakati za wananchi wa Palestina waliokuwa wakihudhuria mazishi ya wenzao wawili waliouawa shahidi na askari katili wa utawala huo bandia katika maandamano ya amani katika Ukanda wa Gaza.

Habari zaidi zinasema kuwa, jeshi la Israel limekiri kutunguliwa kwa ndege yake hiyo ya kijasusi, lakini limejitetea kuwa hakuna wasiwasi wa kuvuja taarifa za kiintelijensia zilizokuwa kwenye drone hiyo.

Wapalestina wakiwazika wenzao waliouawa shahidi na Israel

Hapo jana Wapalestina wa mji wa Khan Yunis walifanya maandamano ya amani kabla ya kuwazika wenzao wawili akiwemo kijana aliyekuwa na umri wa miaka 13 kwa jina Yaser Amjad Abu Naja, waliouawa shahidi na wanajeshi katili wa Israel siku ya Ijumaa katika maandamano ya 'Haki ya Kurejea'.

Hadi sasa Wapalestina zaidi ya 140 wameuliwa shahidi kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel kwenye maandamano hayo na wengine zaidi ya elfu 15 wamejeruhiwa. Maandamano ya 'Haki ya Kurejea' yalianza tarehe 30 mwezi Machi.