Uchunguzi: Israel ilimuua muuguzi wa Kipalestina Gaza kwa makusudi
Uchunguzi uliofanywa na shirika moja la kutetea haki za binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu umesema jeshi katili la utawala wa Kizayuni wa Israel lilimuua kwa makusudi muuguzi wa Kipalestina katika Ukanda Ghaza.
Kituo cha Kizayuni kinachojulikana kwa jina la B'Tselem kimesema muuguzi huyo wa Kipalestina alipigwa risasi na kuua na wala hakikuwa kisa cha bahati mbaya kama inavyodaiwa.
Amit Gilutz, msemaji wa kituo hicho amesema, "Najjar alikuwa amesimama umbali wa mita 25 kutoka uzio wa Gaza, wakati alipolengwa na kufyatuliwa risasi kwa makusudi na askari wa Israel, na madai yaliyotolewa na jeshi la Israel kuwa aliuawa kwa bahati mbaya hayana msingi."
Razan al-Najjar, muuguzi wa kujitolea aliyekuwa na umri wa miaka 21 na aliyekuwa akiifanyia kazi Wizara ya Afya ya Gaza, licha ya kwamba alikuwa amevalia sare rasmi za kazi, lakini aliuawa shahidi kwa kufyatuliwa risasi kifuani, alipokuwa akiwapa matibabu waandamanaji wa Gaza waliojeruhiwa Ijumaa ya Juni Mosi.
Mohammad Javad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alilaani kitendo cha utawala wa Kizayuni wa Israel cha kumuua shahidi muuguzi wa Kipalestina katika Ukanda wa Ghaza, na kuutaja ukatili huo kama doa jingine kwa utawala huo haramu.
Tangu tarehe 30 Machi mwaka huu yalipoanza maandamano ya Haki ya Kurejea, Wapalestina zaidi ya 140 wameuawa shahidi na wengine elfu 15 kujeruhiwa na wanajeshi katili wa Israel.