Ansarullah: Tuko tayari kuikabidhi UN usimamizi wa al Hudaydah kwa sharti
Harakati ya wananchi ya Ansarullah nchini Yemen imesema itakubali kukabidhi usimamizi wa bandari ya al Hudaydah kwa Umoja wa Mataifa, lakini kwa sharti.
Katika mahojiano na gazeti la Ufaransa la Le Figaro, Abdul Malik al Houthi, Katibu Mkuu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema, "Nimemtaarifu Martin Griffiths, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen juu ya utayarifu wetu wa kukabidhi usimamizi wa al Hudaydah kwa taasisi hiyo ya kimataifa kwa sharti kwamba, uvamizi dhidi ya bandari hiyo ya kistratajia usitishwe."
Amebainisha kuwa, haiyumkiniki kuwashurutisha Wayemen waondoke katika mji wao wa al-Hudaydah na kuukabidhi Umoja wa Falme za Kiarabu unaotenda jinai dhidi ya Wayemen na kuongeza kuwa, matakwa hayo yanakiuka mikataba ya kimataifa.
Amefafanua kuwa, "Ni sawa na Uingereza kuitaka Ufaransa iondoke Paris na kuukabidhi mji huo kwa serikali ya London. Ni jambo lisilokuwa na mantiki."
Hivi karibuni, Martin Griffiths, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen alifanya ziara Sana'a, mji mkuu wa nchi hiyo na kukutana na viongozi wa serikali ya wokovu wa kitaifa.
Wanajeshi vamizi katika muungano vamizi unaoongozwa na Saudia na unaopata himaya ya Marekani, Uingereza na Ufaransa, mnamo Juni 13 ulipuuza tahadhari ya Umoja wa Mataifa kuhusu kuhatarishwa maisha ya malefu ya raia mjini al Hudayda na kuanzisha hujuma kali ya anga, nchi kavu na baharini dhidi ya eneo hilo.
Tangu Wasaudia walipoanzisha mashambulizi ya kivamizi dhidi ya nchi maskini ya Yemen mwezi Machi 2015, bandari ya al Hudayda iko mikononi mwa kamati za kujitolea za wananchi wa nchi hiyo.