Fawzi Barhoum: Kunyamazia mashambulio ya Israel ni jambo lisilokubalika
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i47032-fawzi_barhoum_kunyamazia_mashambulio_ya_israel_ni_jambo_lisilokubalika
Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema kuwa, kunyamazia kimya hujuma na mashambulio ya utawala unaomwaga damu na unaotenda jinai wa Israel ni jambo lisilokubalika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 26, 2018 09:55 UTC
  • Fawzi Barhoum: Kunyamazia mashambulio ya Israel ni jambo lisilokubalika

Msemaji wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema kuwa, kunyamazia kimya hujuma na mashambulio ya utawala unaomwaga damu na unaotenda jinai wa Israel ni jambo lisilokubalika.

Fawzi Barhoum amesema hayo katika ujumbe wake aliouandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter na kusisitiza kwamba, Wapalestina hawatanyamazia kimya na kuyaangalia tu mashambulio ya utawala haramu wa Israel bali watatoa majibu yanayofaa kwa uchokozi na jinai hizo za Israel.

Msemaji wa HAMAS amesisitiza kuwa, adui anapaswa kutambua kwamba, atalipa gharama ya jinai zake na hatua zake za kumwaga kiholela damu za wapiganaji na wananchi madhulumu wa Palaestina.

Brigedi ya Shahidi Izzuddin Qassam tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS imetangaza kuwa, itatoa majibu yanayofaa na kulipiza kisasi jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Hujuma za Israel dhidi ya Gaza

Kwa akali Wapalestina watatu wameuawa shahidi katika wimbi jipya la mashambulizi ya angani na nchi kavu ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya makazi ya raia katika Ukanda wa Gaza. 

Utawala huo haramu umedai kuwa mashambulizi hayo ni ya kulipiza kisasi kutokana na risasi zilizofyatuliwa kutoka ukanda ulio chini ya mzingiro wa kibaguzi na kidhalimu. 

Tokea Machi 30 hadi sasa, Wapalestina karibu 150 wameuawa shahidi katika maandamano hayo ya amani baada ya kufyatuliwa risasi na wanajeshi wa utawala katili wa Israel huku wengine karibu 16,000 wakijeruhiwa.