Jibu la Wapalestina kwa uharamia wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i47153-jibu_la_wapalestina_kwa_uharamia_wa_israel
Mkuu wa Idara ya Siasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) Ismail Hania ametoa ujumbe akilaani shambulizi la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya meli iliyokuwa njiani ikielekea Ukanda wa Gaza kuvunja mzingiro wa Israel dhidi ya wakazi wa eneo hilo na vilevile uharamia wa askari wa Israel wa kuwashambulia wanaharakati wa kimataifa wanaolitetea taifa la Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 01, 2018 01:41 UTC
  • Jibu la Wapalestina kwa uharamia wa Israel

Mkuu wa Idara ya Siasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) Ismail Hania ametoa ujumbe akilaani shambulizi la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya meli iliyokuwa njiani ikielekea Ukanda wa Gaza kuvunja mzingiro wa Israel dhidi ya wakazi wa eneo hilo na vilevile uharamia wa askari wa Israel wa kuwashambulia wanaharakati wa kimataifa wanaolitetea taifa la Palestina.

Wanaharakati 40 na shakhsia wa kimataifa kutoka nchi 15 za dunia walikuwa katika meli hiyo ya Al Awda iliyokuwa mbioni kuelekea Gaza kwa ajili ya kuvunja mzingiro wa Israel na kuwafikishia misaada ya dharura raia wanaoteseka wa Gaza. Hata hivyo askari wa utawala katili wa Israel waliishambulia meli hiyo na kukatiza safari yake sambamba na kutwaa misaada yote ya kibinadamu iliyokuwemo. Meli hiyo pia ilichukuliwa na askari wa Israel na kupelekwa katika bandari ya Ashdod.

Kamati ya Kimataifa ya Kuvunja Mzingiro wa Gaza imetangaza kuwa, wanaharakati 20 wa kimataifa waliokuwa ndani ya meli ya hiyo wanaendelea kushikiliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel. Meli hiyo ni moja katika msafara wa Meli za Uhuru zinazolenga kuvunja mzingiro Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.

Askari wa Israel wanawaua wanaharakati wa misaada ya kibinadamu

Hii si mara ya kwanza kwa Israel kusimamisha na kuteka meli ya misaada ya kibinadamu kwa ajili ya raia wa Gaza. Mwezi Mei mwaka 2010 makamondoo wa Jeshi la Majini la Israel walishambulia meli ya Marmara ya Uturuki iliyokuwa ikikaribia pwani ya Gaza ikiwa na misaada ya kimataifa ya kibinadamu na kuwaua au kuwajeruhi makumi ya wanaharakati wa haki za binadamu waliokuwemo. Yapata miaka mitatu iliyopita pia askari wa Israel walishambulia meli ya Marianne kutoka Sweden iliyokuwa na misaada ya kibinadamu kwa ajili ya watu wa Gaza na kuitwaa. Meli hiyo ilikuwa sehemu ya msafara wa meli kadhaa za kuvunja mzingiro wa Gaza uliopewa jila la Freedom Flotilla III. 

Tangu mwezi Januari mwaka 2006 na baada ya harakati ya Hamas kushinda uchaguzi wa Bunge la Palestina, Israel iliweka mzingiro wa anga, baharini na nchi kavu dhidi ya raia wa eneo hilo kwa shabaha eti ya kuiondoa madarakani harakati hiyo ya mapambano ya ukombozi wa Palestina. 

Hali ya sasa ya Palestina inaonesha kuwa, juhudi za wanaharakati wa kimataifa za kutaka kuvunja mzingiro huo zitaendelea hadi pale utawala haramu wa Israel utakaposalimu amri. Hatua zinazochukuliwa na watu kutoka nchi mbalimbali za dunia kwa ajili ya kuwasaidia raia wanaoteseka wa Ukanda wa Gaza kupitia njia mbalimbali ikiwemo ya kutuma meli za misaada ya kibinadamu, zimezidisha mazingatio ya walimwengu kuhusu mgogoro wa Palestina. Si hayo tu bali kitendo cha kutuma meli zenye misaada ya kibinadamu huko Gaza pekee kinatoa ujumbe kwa wakazi wa eneo hilo kwamba, walimwengu hawawezi tena kuvumilia ukatili wa utawala ghasibu wa Israel na kwamba raia wa Gaza hawako peke yao katika masaibu hayo. Vilevile kitendo hicho kinatoa ujumbe kwamba, jamii ya kimataifa na watu huru hawaogopi vitisho vya utawala wa kigaidi wa Israel na wataendeleza jitihada zao hadi mzingiro huo utakapovunjwa. Lengo jingine la kutuma meli za misaada ya kibinadamu kwa watu wa Gaza ni kutaka kuamsha na kuzindua jumuiya za kimataifa zinazotazama kwa macho tu maafa na masaibu ya watu wa Palestina na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaoendelea kufanywa na Israel katika eneo hilo.

Watoto wa Gaza wanaendelea kuteseka kutokana na mzingiro wa Israel

Ukweli ni kwamba shambulizi la Israel dhidi ya meli zinazobeba misaada ya kimataifa kwa watu wa Gaza ambazo zinaelelekea katika eneo hilo kupitia bandari za kimataifa na kwa njia za kisheria, ni uharamia wa wazi dhidi ya wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wanaotetea haki za taifa la Palestina. Mienendo ya Israel dhidi ya meli zenye misaada ya kibinadamu zinazoelekea Gaza inawakumbusha walimwengu maharamia hatari wa karne zilizopita, na suala hili linaweka wazi zaidi sura na utambulisho halisi wa utawala bandia na pandikizi wa Israel.