Wazayuni wachochea vita zaidi dhidi ya Wapalestina
Licha ya kuweko onyo la kimataifa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusu jinai zake dhidi ya Wapalestina, baraza la mawaziri la utawala huo dhalimu jana usiku liliitisha kikao maalumu na kutaka mashambulizi dhidi ya wananchi wa Ghaza yaendelee.
Redio moja ya utawala wa Kizayuni imetangaza habari hiyo na kusema kuwa, baraza la mawaziri la kisiasa na kiusalama la Israel limelitaka jeshi la utawala huo kushadidisha mashambulizi yake dhidi ya Ukanda wa Ghaza.
Wimbi jipya la mashambulizi ya ndege za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Ghaza lilianza usiku ya juzi Jumatano.
Ufaransa na Ujerumani zimeelezea kusikitishwa kwao na kuongezeka mapigano katika Ukanda wa Ghaza na kutaka mapigano hayo yasimamishwe mara moja.
Jioni ya jana pia, ndege za utawala wa Kizayuni wa Israel zilishambulia kituo kimoja cha kiutamaduni huko Ghaza na kujeruhi Wapalestina wasiopungua 18.
Utawala wa Kizayuni umekiri pia kuwa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vimeshambuliwa kwa makombora 150 ya makundi ya wanamapambano wa Palestina na kwamba ngao ya kujilinda na makombora ya Israel inayoitwa 'ngao ya chuma' imefanikiwa kuangusha makombora 25 tu.
Mashambulizi ya kivamizi ya Israel dhidi ya eneo lililozingirwa kila upande la Ghaza yamekuja katika hali ambayo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS hivi sasa inafanya mazungumzo na mwakilishi wa Umoja wa Mataifa na viongozi wa Misri kuhusu kuongezwa muda wa kusimamishwa mapigano.