Aug 25, 2018 14:23 UTC
  • Russia yaionya Marekani kuhusiana na chokochoko ya aina yoyote nchini Syria

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia imeionya Marekani kuhusiana na chokochoko ya aina yoyote ile nchini Syria.

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia iliyotolewa leo imesisitiza kuwa, Moscow inaionya Washington kuhusiana na hatua yoyote ile ya kuzusha chokochoko huko nchini Syria.

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia inatoa onyo hilo katika hali ambayo, Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo  imetoa taarifa juu ya kuweko mikakati ya  magaidi walioko Syria ya kufanya shambulio la silaha za kemikali na hivyo kupatikana kisingizio cha kushambuliwa kijeshi Syria kwa madai kwamba, vikosi vya Syria ndivyo vilivyotekeleza shambulio hilo.

Rais Bashar al-Assad wa Syria

Wizara ya Ulinzi ya Russia imefichua kwamba, Marekani, Uingereza na Ufaransa zikiwa na lengo la kutekeleza njama zao zinapanga mkakati wa kufanyika shambulio la silaha za kemikali nchini Syria na kulituhumu jeshi la nchi hiyo kwamba, ndilo lililohusika na shambulio hilo.

Itakumbukwa kuwa, Aprili mwaka huu, Marekani, Uingereza na Ufaransa zilifanya mashambulio ya makombora katika maeneo mbalimbali ya Syria baada ya tukio la kutiliwa shaka la shambulio la silaha za kemikali.

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Ryabkov amesema kuwa nchi yake inaheshimu uwepo wa Iran nchini Syria kwani iko huko kihalali na kwa mwaliko wa serikali halali ya nchi hiyo inayoongozwa na Rais Bashar al-Assad.

Tags