Ismail Hania ataka kuhitimishwa masaibu na machungu ya taifa la Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i48408-ismail_hania_ataka_kuhitimishwa_masaibu_na_machungu_ya_taifa_la_palestina
Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ameyataka mataifa ya dunia, kufanya hima kwa ajili ya kuhitimisha masaibu na machungu wanayokabiliwa nayo wananchi madhulumu wa Palestina.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 26, 2018 23:29 UTC
  • Ismail Hania ataka kuhitimishwa masaibu na machungu ya taifa la Palestina

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) ameyataka mataifa ya dunia, kufanya hima kwa ajili ya kuhitimisha masaibu na machungu wanayokabiliwa nayo wananchi madhulumu wa Palestina.

Ismail Hania amesema hayo katika Ukanda wa Gaza katika shughuli ya kuusindikiza mwili wa mmoja wa mashahidi wa Palestina na kueleza kwamba, katika maeneo ya Ukanda wa Gaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, Quds, ardhi zilizokaliwa kwa mabavu mwaka 1948 na katika kambi za wakimbizi wa Kipalestina kuna raia wanaoishi ambao wanafungamana na haki zao, taifa lao na Quds Tukufu.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesisitiza kuwa, maandamano makubwa ya 'Haki ya Kurejea' yataendelee hadi pale malengo yote yatakapofikiwa ambapo kubwa zaidi likiwa ni kuvunja mzingiro dhidi ya Gaza.

Ismail Hania amesema wazi kuwa, taifa la Palestina limeingia katika vita vya kuuvunja mzingiro na kuunga mkono misingi yake ya kitaifa na kwamba, katu halitaacha au kusitisha vita hivyo.

Taswira ya mshikamano wa Wapalestina katika Maandamano ya 'Haki ya Kurejea'

Maandamano ya amani yaliyopewa jina la "Haki ya Kurejea" yalianza tarehe 30 Machi mwaka huu kwa mnasaba wa Siku ya Ardhi huko Ukanda wa Gaza na yangali yanaendelea.

Tangu wakati huo hadi sasa zaidi ya Wapalestina 150 wameuawa shahidi kwa kupigwa risasi na askari wa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na wengine 17,500 wamejeruhiwa. Maandamano hayo yamewatia kiwewe viongozi wa utawala dhalimu wa Israel na ndio maana wamekuwa wakiwafyatulia risasi waandamanaji na kuwaua ovyo.