Stratijia ya Wapalestina kwa ajili ya kukabiliana na "Muamala wa Karne"
Vyama na makundi ya mapambano ya ukombozi wa Palestina Jumatano iliyopita yaliandika na kutayarisha mpango wa "Uokovu wa Taifa" kwa ajili ya kukabiliana na kile kilichopewa jina la "Muamala wa Karne" uliotayarishwa na Marekani kwa shabaha ya kumaliza kabisa kadhia ya Palestina.
Harakati ya Kidemokrasia ya Ukombozi wa Palestina, Harakati ya Wapalestina kwa Ajili ya Ukombozi, Jumuiya ya Sai'qa, Jihad Islami na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) zimetia saini hati hiyo ya Uokovu wa Kitaifa. Hati hiyo inasisitiza kuwa, mapambano ya ukombozi ni mstari mwekundu ambao hakuna mtu anayepasa kuuvuka na kwamba mapambano ya silaha ya Wapalestina dhidi ya maghasibu Wazayuni yataendelea maadamu ardhi ya Palestina inaendelea kukaliwa kwa mabavu.
Mpango wa Wapalestina kwa ajili ya kukabiliana na njama ya Muamala wa Karne umetangazwa baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kutangaza Jumatano iliyopita kwamba, mwenendo mpya wa mazungumzo baina ya Wapalestina na Israel katika kalibu ya Muamala wa Karne, utaanza miezi miwili hadi mitatu ijayo.
Trump amesisitiza katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel huko New York kwamba, Marekani daima itaendelea kuwa pamoja na Israel. Trump ametetea ukatili na jinai zinazofanywa na Israel huko Palestina kwa kudai kuwa, Tel Aviv inalazimika kutumia mabavu dhidi ya Wapalestina kutokana na hali ngumu ya Mashariki ya Kati. Uungaji mkono huu mkubwa wa Marekani kwa jinai na ukatili wa Israel dhidi ya raia wa Palestina una maana ya kuuruhusu utawala huo kuendeleza unyama na mauaji katika eneo la Mashariki ya Kati. Vilevile mpango wa Trump wa eti Muamala wa Karne unatayarisha mazingira mazuri zaidi kwa Israel kwa ajili ya kutimiza ndoto yake ya kudhibiti ardhi zote zinazoanzia mto Nile hadi Furati.
Wakati huo huo Rais Michel Aoun wa Lebanon amekosoa mienendo ya Marekani kuhusu Palestina na kusema: Washington inafanya mikakati ya kuharibu kabisa utambulisho wa Palestina. Aoun ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York ameashiria uamuzi wa Marekani wa kukata misaada yake kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Palestina (UNRWA) kusema: Lengo la hatua hiyo ya serikali ya Washington ni kutokomeza kikamilifu utambulisho wa Palestina na kuwazuia wakimbizi wa Palestina kurejea katika nchi yao iliyoghusubiwa.
Katika kipindi cha sasa ambapo Rais wa Marekani anafanya kila awezalo kukanyaga haki za Wapalestina, inaonekana kwamba kuna udharura wa kuchukuliwa hatua madhubuti zaidi za kukabiliana na mipango ya White House inayotekelezwa kupitia kile kilichopewa jina la Muamala wa Karne. Ni kutokana na hali hiyo ndipo makundi ya mapambano ya Palestina, sawa yale ya Kiislamu au ya kitaifa, yakakutana na kubuni mpango wa Uokovu wa Kitaifa na kutilia mkazo udharura wa kudumishwa mapambano ya silaha dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel. Mbali na hayo mshikamano wa makundi yenye mielekeo na mirengo mbalimbali ya Palestina katika kipindi cha sasa ni ishara ya kushindwa sera za serikali ya Donald Trump za kutaka kuzusha hitilafu kati ya makundi hayo, kuyagawa na kisha kuwatwisha Wapalestina mpango hatari wa Muamala wa Karne.
Maamuzi ya kistratijia ya makundi ya mapambano ya ukombozi ya Palestina kwa hakika yanaakisi mitazamo ya Wapalestina wote ya kupinga mpango wa Trump na vibaraka wake wa Kiarabu kama Saudi Arabia na Imarati. Hali hii inaonesha kuwa, mpango wa Trump wa "Muamala wa Karne" umezaliwa ukiwa umekufa na hauna mteja kati ya watu wa Palestina na mataifa mengine ya eneo la Mashariki ya Kati.