Al Sisi atetea hatua ya kuipatia Saudia visiwa viwili
Rais wa Misri ametetea uamuzi wa serikali ya nchi hiyo wa kuikabidhi Saudi Arabia visiwa viwili.
Rais Abdel Fattah al Sisi wa Misri leo ametetea uamuzi wa serikali ya nchi hiyo wa kuikabidhi Saudi Arabia visiwa viwili vya kistratejia vilivyoko katika bahari Nyekundu na kudai kuwa, Cairo haijauza ardhi yake, bali imerewarejeshea Wasaudia haki yao.
Serikali ya Misri imetangaza kuwa visiwa vya Tiran na Sanafir ambavyo viko katika Ghuba ya Aqaba ni milki ya Saudi Arabia.
Wananchi wa Misri wameituhumu serikali na viongozi wa nchi hiyo kuwa ni wauzaji wa ardhi kwa Saudia. Wakati huo huo Samih Shoukri Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri ametangaza kuwa makubaliano ya kuainisha mipaka ya baharini kati ya nchi hiyo na Saudi Arabia ambayo kwa mujibu wake visiwa viwili vya Tiran na Sanafir ni mali ya Saudia; hayatatekelezwa kabla ya kuchukuliwa hatua za lazima kwa mujibu wa katiba ya Misri. Shoukri ameongeza kuwa ili kuweza kutekelezwa, makubaliano hayo kwanza yanapasa kuidhinishwa na bunge la Misri na kisha kusainiwa na rais. Hatua ya Misri ya kukiri kwamba visiwa hivyo viwili ni milki ya Saudia imekabiliwa na upinzani wa hata waungaji mkono wa serikali ya Rais Abdel Fattah al Sisi mwenyewe.