Lieberman akiri, maandamano ya Haki ya Kurejea yametoa pigo kwa Israel
-
Avigdor Lieberman
Waziri wa Vita aliyejiuzulu wa Israel amekiri kwamba, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imetoa mashinikizo makubwa kwa utawala huo kupitia maandamano yanayofanywa kila siku ya Ijumaa na raia wa Ukanda wa Gaza huko Palestina.
Avigdor Lieberman amesema kuwa, maandamano hayo yaliyopewa jina la Haki ya Kurejea yameilazimisha Israel ichukue 'hatua ya kijinga' na kusalimu amri mbele ya Hamas kwa kuruhusu kupelekwa nishati katika eneo la Gaza.
Waziri wa zamani wa vita wa Israel amekiri kuwa, nafasi ya sasa ya Israel mkabala wa harakati ya Hamas ni mbaya na isiyokubalika na kwamba, Hamas imepata mafanikio makubwa ya kiuchumi kupitia maandamano ya Haki ya Kurejea, suala ambalo ni maafa kwa Israel.
Avigdor Lieberman alilazimika kujiuzulu uwaziri wa vita wa Israel katikati ya mwezi uliopita wa Novemba kutoka na mashambulizi makali ya zaidi ya makombora 400 ya wanapambano wa Palestina yaliyolenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na vituo vya jeshi la Israel.
Ni vyema kuashiria hapa kwamba, tangu tarehe 30 Machi Wapalestina raia wa Ukanda wa Gaza wamekuwa wakifanya maandamano makubwa kila siku ya Ijumaa katika mpaka wa eneo hilo na ardhi inayokaliwa kwa mabavu na Israel wakitaka kufutwa mzingiro wa Gaza na kurejea wakimbizi wa kipalestina katika nchi yao.