Saudi Arabia; kituo cha wafungwa wa kiusalama katika ulimwengu wa Kiarabu
Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia imetangaza kuwa nchi hiyo ina wafungwa wa kiusalama zaidi ya 5,400.
Saudi Arabia ni moja ya nchi zinazokiuka pakubwa haki za binadamu. Muundo wa kisiasa wa nchi hiyo unafanana na utawala wa kidikteta wa moja kwa moja. Katika mfumo huo kila kitu hudhibitiwa na serikali ambapo haki za mtu binafsi khususan katika uga wa kisiasa hazina maana, upinzani na ukosoaji wowote hukabiliwa na adhabu kali huku jela zake zikiwa zimejaa wafungwa wa makosa yanayotajwa kuwa ya kuhujumu usalama.
Katika uwanja huo, wizara mbili za Saudi Arabia zimekiri kuhusu kuwepo wafungwa hao wa makosa ya kiusalama. Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo imetangaza kuwa kuna zaidi ya wafungwa wa kuhujumu usalama zaidi ya 5,400 nchini humo na kwa mujibu wa tangazo la Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo pia katika kipindi cha chini ya mwezi mmoja uliopita watu 65 wametiwa nguvuni kwa kile kilichotajwa kuwa uhalifu wa kiusalama; ambapo 46 miongoni mwao ni raia wa Saudia.
Mbali na kuwa mfumo wa kisiasa ndio unaosababisha hali ya nchi hiyo kuwa ya kiusalama na kipolisi, lakini pia ukoo na ukabila katika idara za nchi hiyo umechangia pakubwa kudhihiri kwa hali hiyo.

Ukoo wa kifalme wa Aal Saud ndio unaoshikilia madaraka nchini Saudia. Katika fremu hiyo, hata ukosoaji wowote ndani ya ukoo huo wa kifalme pia hukabiliwa na radiamali ya kimabavu kutoka kwa utawala ulioko madarakani; na wanawafalme ambao hujaribu kukosoa hali iliyopo na siasa zinazoendeshwa na utawala wa Aal Saud hukabiliwa na hatua kali za kisheria na kiusalama kutoka kwa watawa walioko madarakani.
Aidha taathira za mafunzo ya Kiwahabi pia zimekuwa na nafasi kuu katika kuufanya muundo wa utawala wa Saudia kuwa wa kimabavu. Kuwepo mfungamano kati ya utawala wa Aal Saud na Uwahabi kumepelekea kushtadi mienendo ya utumiaji mabavu na ukandamizaji nchini humo. Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa mafundisho ya Uwahabi, hatua yoyote ya kupinga na kuukosoa mfumo ulioko madarakani inahesabiwa kuwa ni uhalifu. Ni dhahir shahir kwamba moja ya sababu zinazoupelekea utawala wa Aal Saud kutekeleza hatua hizo za ukandamizaji na kuchochea vita nje ya mipaka yake pia ni mienendo hiyohiyo uliorithi ya Kiwahabi.

Sababu nyingine yenye nafasi katika kusababisha kuongezeka wafungwa hao wanaotajwa kuwa wa kuhujumu usalama huko Saudia ni namna madola ajinabi yanavyoamiliana na Riyadh. Madola ajinabi khususan Marekani hayana mtazamo wa kawaida kwa Saudia bali zaidi yanaitazama nchi hiyo kama wenzo wa kimaslahi na kimaada tu. Mtazamo wa aina hii una nguvu kubwa katika siasa za viongozi wa madola hayo, khususan katika siasa za Rais Donald Trump wa Marekani. Maslahi ya madola hayo yamekita mizizi hasa katika sekta tatu za mafuta, mauzo ya silaha na uungaji mkono kwa utawala haramu wa Israel, ambapo masuala muhimu ya demokrasia, haki za binadamu na matatizo mengine mengi ya pamoja yanayoikumba jamii ya mwanadamu hutolewa mhanga na kupuuzwa kwa ajili tu ya kutetea na kuulinda utawala kibaraka wa Saudia.
Wahanga wakuu wa hali hiyo ya kusikitisha ni wananchi wa Saudia ambao, chini ya kimya cha madola ya Magharibi na jamii ya kimataifa, hukabiliwa na kila aina ya ukandamizaji huku watawala wakiibadilisha nchi hiyo kuwa jela kwa ajili ya raia wake.

Hata kama siasa za mabavu za watawala wa Saudia huwakumba raia wote wa nchi hiyo lakini kundi la Mashia ndilo linalokabiliwa na sehemu kubwa ya ukandamizaji huo. Nukta ya mwisho ni kwamba muamala wa kiusalama na kipolisi dhidi ya raia wa Saudi Arabia hauzingatii sheria zozote za kibinadamu ambapo raia hao huwekwa korokoroni kwa miaka mingi bila ya kufikishwa mahakamani. Kwa mujibu wa ripoti za shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch, wafungwa hao wa Sauda huzuiliwa korokoroni kwa kipindi cha hata zaidi ya miaka 10 bila kuhukumiwa.