Magereza ya Uingereza; uwanja wa kujifaragua magenge ya uhalifu
(last modified Wed, 15 Jan 2025 07:38:48 GMT )
Jan 15, 2025 07:38 UTC
  • Magereza ya Uingereza; uwanja wa kujifaragua magenge ya uhalifu

Mkaguzi Mkuu wa Magereza nchini Uingereza ametahadharisha kuwa matumizi ya ndege zisizo na rubani (droni) kuingiza silaha na mihadarati katika magereza ya nchi hiyo ni tishio kwa usalama wa taifa licha ya ulinzi mkali uliopo.

Charlie Taylor, Mkuu wa Idara ya Ukaguzi wa Magereza nchini Uingereza jana aliarfu kuwa jela za Manchester na Long Lartin, zenye wahalifu hatari zaidi wakiwemo magaidi na vinara wa magenge mbalimbali ya uhalifu  zinakabiliwa na mgogoro mkubwa wa biashara mbalimbali haramu zinazofanywa na ndege zisizo na rubani. 

Ukaguzi uliofanywa katika magereza za Manchester na Long Lartin unaonyesha kuwa ndege zisizo na rubani zinatumika kubeba mizigo mikubwa zaidi ya madawa ya kulevya, simu za mkononi na hata silaha, huku baadhi ya wafungwa wakiziongoza ndege zisizo na rubani kwenye seli zao kwa kuchoma madirisha ya magereza ili kupokea dawa za kulevya na silaha.

Magareza za Uingereza na uhalifu wa madawa ya kulevya na silaha 

Taylor amesisitiza kuwa, uchumi haramu umestawi katika magereza hayo, na magenge ya wahalifu yanadhibiti hali ya mambo karibu na magereza hayo. Katika ripoti yake, Taylor ameitaka Wizara ya Sheria ya Uingereza kuchukua hatua haraka iwezekanavyo ili kukabiliana na uhalifu huu tajwa.

Mkuu wa Idara ya Ukaguzi wa Magereza ya Uingereza amesema: "Inatia wasiwasi sana kuona polisi na idara ya magereza zinashindwa kusimamia na kufuatilia hali ya mambo katika maeneo ya magereza hayo."