Hali ya haki za binadamu Bahrain ni mbaya sana
(last modified Wed, 13 Feb 2019 02:32:24 GMT )
Feb 13, 2019 02:32 UTC
  • Hali ya haki za binadamu Bahrain ni mbaya sana

Kamati ya Kimatiafa ya Haki za Binadamu Eneo la Asia Magharibi imesema hali ya haki za binadamu inazidi kuwa mbaya nchini Bahrain ambapo ukoo wa Aal Khalifa ambao unatawala nchi hiyo umehusika na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Hayo yamedokezwa na Haitham Abu Saeed katika mahojiano na Shirika la Habari la Mehr na kuongeza kuwa: "Wakuu wa Bahrain hawaheshimu hata kidogo mikataba ya kimataifa ambayo wameitia saini na wala hawashirikiani na maafisa wa haki za binadamu wanaotaka kuchunguza hali katika magereza ya kuogofya nchini humo."

Ameongeza kuwa madola ya kigeni, hasa Saudi Arabia, yameingia kijeshi Bahrain kwa kisingizio cha muungano wa 'Ngao ya Rasi' na hivyo kupelekea ukandamizaji kuongezeka nchini humo. Abu Saeed amesema vyombo vya mahakama vya utawala wa Aal Khalifa vinawatesa sana wafungwa kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa.

Aidha Abu Saeed amesema kutolewa hukumu ya kifungo cha maisha kwa Sheikh Ali Salman, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kiislamu ya Al Wifaq ni ishara ya kuendelea mashinikizo ya kisiasa nchini humo.

Maandamano nchini Bahrain

Tangu Februari 14 mwaka 2011 hadi sasa, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa kiukoo wa Aal Khalifa.

Wananchi hao wanataka kuwepo uhuru, utekelezwe uadilifu, ukomeshwe ubaguzi na kuundwa serikali itakayochaguliwa na wananchi wenyewe.

Hata hivyo kwa msaada wa wanajeshi wa Saudi Arabia na askari usalama wa Imarati waliotumwa nchini Bahrain, utawala wa Aal Khalifa unatumia mkono wa chuma kukabiliana na matakwa ya wananchi hao.

Kwa mujibu wa duru za haki za binadamu, Bahrain ina idadi kubwa zaidi ya wafungwa wa kisiasa kulinganisha na idadi ya watu katika nchi hiyo ndogo zaidi katika Ghuba ya Uajemi.