Mar 12, 2019 07:45 UTC
  • Zarif: Marekani haiwezi kuzuia kustawi uhusiano wa Iran na Iraq

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Marekani haina uwezo wa kusimamisha uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu na Iraq, na kwamba serikali ya Baghdad imejenga uhusiano huo katika misingi ya matakwa na maslahi ya taifa hilo.

Muhammad Javad Zarif aliyasema hayo jana mjini Baghdad katika mahojiano na shirika la habari la BBC ya Kiarabu na kubainisha kuwa, "Tuna uhusiano mzuri na Iraq. Iraq ni jirani yetu. Hata vita vilivyoanzishwa na dikteta Saddam Hussein dhidi ya Iran kati ya mwaka 1980-88 havikuweza kuyatenganisha mataifa haya mawili."

Amefafanua kuwa, uhusiano wa nchi mbili hizi umejengeka katika misingi ya udugu, historia, jografia, utamaduni na hata udugu wa kifamilia.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi za juu wa Iran ameongeza kuwa, usalama na uthabiti wa Iraq una umuhimu mno kwa Iran kwani Iraq yenye utulivu inaweza kuwa na nafasi muhimu katika eneo.

Iran na Iraq zimesaini Mikataba 5 ya Maelewano katika nyuga za uchumi na afya 

Dakta Zarif ameandamana na Rais Hassan Rouhani aliyewasili hapo jana Baghdad, mji mkuu wa Iraq akiuongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi wa Iran. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa, "sisi hatujawahi kuitaka Iraq iichague Iran. Washington ndiyo inayoishinikiza Baghdad ichague ima Iran au Marekani."

Tags