Askari wa Israel waua shahidi Wapalestina wawili katika maandamano Ghaza
Wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamewapiga risasi na kuwaua shahidi Wapalestina wawili na kuwajeruhi wengine kadhaa katika Ukanda wa Ghaza wakati wa maandamano ya amani yaliyoitishwa kwa lengo la kuadhimisha kuanza 'Maandamano Makubwa ya Kurejea' na 'Siku ya Ardhi ya Palestina.'
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni za Wizara ya Afya katika Ukanda wa Ghaza, Wapalestina wawili wameuawa shahidi na wengine 59 wamejeruhiwa baada ya kuhujumiwa na wanajeshi wa utawala wa Israel wakati wa maandamano ya amani.
Wanajeshi wa Israel wametumia risasi hai na gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji Wapalestina ambao walikusanyika katika mpaka wa Ukanda wa Ghaza na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni.
"Maandamano Makubwa ya Kurejea' yamekuwa yakifanyika kila wiki tokea Machi 30 mwaka jana na Wapalestina wamekuwa wakitaka utawala wa Kizayuni wa Israel usitishe ukaliaji wa mabavu wa ardhi zao. Aidha wanataka wakimbizi wote Wapalestina warejee katika ardhi zao za jadi.
Siku ya Ardhi maarufu kama "Yaumul Ardh" hufanyika kwa munasaba wa maandamano makubwa yaliyofanyika katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Wapalestina waliitisha maandamano hayo wakitaka utawala wa Kizayuni wa Israel urejeshe ardhi zote ulizopora.