Muungano vamizi wachoma moto kijiji kizima Yemen + Video, Picha
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i54156-muungano_vamizi_wachoma_moto_kijiji_kizima_yemen_video_picha
Mamluki wa Saudi Arabia wamechoma moto kijiji kizima katika mkoa wa al Hudaida nchini Yemen na kuongeza orodha ya jinai zao dhidi ya wananchi madhlumu wa Yemen, baada ya wavamizi hao kushindwa katika medani za kivita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 16, 2019 06:28 UTC

Mamluki wa Saudi Arabia wamechoma moto kijiji kizima katika mkoa wa al Hudaida nchini Yemen na kuongeza orodha ya jinai zao dhidi ya wananchi madhlumu wa Yemen, baada ya wavamizi hao kushindwa katika medani za kivita.

Televisheni ya al Masirah ya Yemen imeripoti habari hiyo na kurusha hewani mkanda wa video na picha zinazoonesha kijiji hicho cha eneo la Bayt al Faqih katika mkoa wa al Hudaidah kikiwaka moto baada ya kushambuliwa kwa anga na kwa mizinga ya mamluki wa Saudi Arabia.

Televisheni hiyo imeongeza kuwa, sambamba na mashambulizi hayo ya ndege na mizinga, mamluki hao wa Saudia wamekivamia kijiji hicho na kuchoma moto nyumba za wanakijiji kwa chuki na ukatili mkubwa.

Hii si mara ya kwanza kwa muungano vamizi wa Yemen unaoongozwa na Saudi Arabia kutumia mbinu za utawala wa Kizayuni wa Israel kufanya jinai kubwa kama hiyo. Wavamizi wa Yemen wamewahi kufanya jinai kama hiyo pia katika kijiji walichokizingira cha al Darihami nchini Yemen.

Katika miezi ya hivi karibuni wavamizi hao wanaoongozwa na Saudi Arabia wamepata kipigo kikali kutoka kwa jeshi na kamati za kujitolea za wananchi wa Yemen kwenye medani za mapambano.

Siku ya Jumatano Wayemen waliutwanga kwa kombora aina ya cruse uwanja wa ndege wa Abha wa kusini mwa Saudi Arabia. Siku mbili baadaye yaani Ijumaa asubuhi, Wayemen walituma ndege tano zisizo na rubani kuupiga tena kwa makombora uwanja huo wa Saudia, vipigo ambavyo vimewahamakisha sana wavamizi hao na vibaraka wao.

Mbali na video iliyoambatana na habari hii, hapa chini tumeorodhesha pia picha zinazoonesha sehemu ya jinai hizo za mamluki wa Saudi Arabia nchini Yemen.